Habari

Wasichana wahimizwa washiriki michezo kukwepa mitego ya wanaume

October 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MISHI GONGO

HUKU dunia ikiadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike, wasichana Kaunti ya Mombasa wamehimizwa kujiunga na michezo kujiepusha na ngono za mapema.

Akiongea katika sherehe hizo zilizofanyika katika Uwanja wa Mbuzi mjini Mombasa, Mkurugenzi wa shirika la Coast Women Voice, Bi Halima Mohammed alisema kupitia michezo watoto wa kike wataweza kukabili hisia zao.

“Kupitia michezo watoto wataweza kukabili hisia zao,” akasema.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na wanawake kutoka mashirika mbalimbali akiwemo Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti hiyo Bi Aisha Hussein, Bi Hamisa Zaja mkurugenzi wa shirika la Green Movement na wengineo waliwataka wazazi kuwapa muda zaidi watoto wao.

Mwakilishi wanawake wa kaunti ya Mombasa Bi Aisha Hussein alisema maadili ya watoto yanaendelea kudorora kufuatia wazazi kuwatelekeza watoto wao.

“Wazazi hawana muda na watoto, wanajifunza mengi kupitia simu. Watoto wengi waliopata ujauzito wakidadisiwa husema kuwa watu waliowapachika mimba walipatana nao mitandaoni,” akasema.

Aidha alisema baadhi ya watoto hupachikwa mimba kwa kukosa bidhaa muhimu kama sodo jambo ambalo huwasukuma kwa wanaume.