Msinidharau Mswambweni – Kalonzo
Na CECIL ODONGO
KINARA wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka jana alipuzilia mbali wanaodai kwamba kiny’ang’anyiro cha kuwania ubunge wa Msambweni ni kati ya Naibu Rais Dkt William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga, akisema watashanga chama chake kikinyakua kiti hicho.
Bw Musyoka alieleza imani yake kwamba mwaniaji wa Wiper, Sheikh Mohmoud Abdurahman ni mgombea maarufu ambaye atapita katikati ya mwaniaji wa ODM Omar Boga na mgombeaji huru Feisal Bader, ambaye anavumishwa na Dkt Ruto.
Uchaguzi huo utafanyika Disemba 15 huku wadadisi wakidai kuwa utakuwa jukwaa la Dkt Ruto na Bw Odinga kupimana nguvu, jinsi ilivyokuwa Kibra mwaka jana.
Chama cha Jubilee kilijiondoa kwenye uchaguzi huo ili kumuunga mkono Bw Boga, kikitaja ushirikiano wa ‘handisheki’ kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.
ODM nayo haitakuwa na wagombeaji katika chaguzi ndogo za udiwani kwenye wadi za Kahawa Wendani katika Kaunti ya Kiambu na Lake View katika Kaunti ya Nakuru.
“Tuna mgombeaji ambaye ni maarufu sana na tutampigia kampeni kali. Wale ambao wanaona ushindani huu kama kati ya Raila na Ruto watashangaa. Sisi pia ni Wakenya na tupo tayari kuhakikisha mapenzi ya raia yanatimia kwa kuwashinda wagombeaji wao. Watashangaa kwa sababu mwaniaji wetu ni mtu wa watu,” akasema.
Bw Musyoka alitoa kauli hiyo alipotoa cheti kwa Bw Abdurahman katika makao makuu ya chama hicho mtaani Karen, Nairobi.
Pia alitoa cheti hkwa mwaniaji wa Wiper kwenye uchaguzi mdogo wa wadi ya Kahawa Wendani, Derrick Mbugua na mwenzake wa Wundanyi Mbale katika Kaunti ya Taita Taveta, Stephen Charo.
‘Tutafanya kampeni kwa wawaniaji wote. Tuna kikosi imara na tutashinda,” akaongeza makamu huyo wa rais wa zamani.
Tayari kampeni katika zimeanza mapema Msambweni, huku wawaniaji wakitafuta uungwaji mkono kuchukua nafasi ya aliyekuwa mbunge marehemu Suleiman Dori aliyeaga dunia kutokana na ugonjwa wa saratani mnamo Machi mwaka huu.