ONYANGO: Ajali za barabarani zitaangamiza maelfu ya raia hadi lini?
KUONGEZEKA kwa ajali za barabarani nchini licha ya kuwepo kwa marufuku ya kusafiri usiku na uuzaji wa pombe, kunafaa kushtua serikali.
Katika hotuba yake ya Septemba 28, Rais Uhuru Kenyatta aliwaambia Wakenya kuwa vikwazo vilivyowekwa kuzuia maambukizi ya virusi vya corona – kama vile kafyu, kutojaza abiria kwenye matatu na marufuku ya kuuza pombe –vilisaidia pakubwa kupunguza visa vya uhalifu na ajali za barabarani.
Kwa mujibu wa Rais Kenyatta, visa vya uhalifu vilipungua kwa asilimia 21 kati ya Machi na Septemba. Ajali za barabarani zilipungua kwa asilimia 10 ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho mwaka jana.
Lakini takwimu kuhusu vifo vilivyotokana na ajali za barabarani zilizotolewa hivi karibuni na idara ya polisi, zinatoa taswira tofauti.Takwimu za polisi zinaonyesha kuwa ajali za barabarani zimeongezeka kwa asilimia 1.3 mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana.Watu 2,689 walifariki katika ajali za barabarani kati ya Januari 1 na Septemba 30, mwaka huu.
Watu 2,655 waliangamia katika kipindi sawa na hicho mwaka uliopita.Takwimu hizo zinaonyesha kuwa pikipiki zilisababisha vifo vya watu 1,075 kati ya Januari na Septemba 30, mwaka huu.
Watu 971 waliangamia kwa kukanyagwa na magari au pikipiki mwaka huu. Kenya ilipoteza madereva 233. Watumiaji wa baiskeli 68 pia walipoteza maisha yao barabarani katika kipindi cha miezi tisa iliyopita.
Kwa ufupi, ajali za barabarani zimeua watu wengi zaidi humu nchini kuliko virusi vya corona kati ya Machi na Oktoba.Wengi tulitarajia kuwa mwaka huu ungekuwa na idadi ndogo zaidi ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani. Hii ni kwa sababu kwa miezi saba sasa pamekuwapo kafyu wala magari hayaruhusiwi kusafiri usiku.
Hiyo inamaanisha kuwa ajali hizi zinatokea kati ya alfajiri na jioni. Kwa muda wa miezi sita baa zilikuwa zimefungwa. Uwezekano wa madereva kuendesha magari wakiwa walevi uko chini.
Aidha, magari yamekuwa yakibeba asilimia 60 ya abiria ili watu wasikaribiane katika juhudi za kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.
Hivyo basi, hatuwezi kusema kuwa ajali hizo zinasababishwa na hatua ya matatu kubeba abiria kupita kiasi.Serikali haina budi ila kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kiini cha ajali hizi mbaya za barabarani nchini humu.