Ujasiri mpya wa Ruto
Na BENSON MATHEKA
NAIBU Rais William Ruto ameanza kuonyesha ujasiri wa kipekee kwa kuelekeza mishale yake moja kwa moja kwa Rais Uhuru Kenyatta huku uhasama kati ya wawili hao ukikolea licha ya juhudi za viongozi wa makanisa kuwapatanisha.
Ingawa awali, Dkt Ruto alikuwa akiepuka kumshambulia Rais moja kwa moja katika mikutano yake ya kisiasa, kauli zake katika mikutano ya hivi majuzi zimekuwa zikimlenga kiongozi wa nchi.
Akiwa Nyamira Jumatano wiki jana, Dkt Ruto alilaumu mchakato wa kubadilisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), kauli ambayo ilionekana kumlenga rais ambaye amekuwa msitari wa mbele kushinikiza marekebisho ya katiba.
“Wanasema eti tubadilishe katiba kuwe na Waziri Mkuu… sisi tunasema tubadilishe mjadala tuanze kuongea kuhusu mwananchi mdogo. Wakikuja na mambo ya viongozi tutawaambia tunataka mambo ya wananchi, wakikuja na mambo ya mamlaka tutawaambia tunataka kazi kwa mwananchi mdogo,” alisema Ruto.
“Mimi si wazimu na mimi si mjinga na mimi si mlevi… Mimi ninajua kile ninasema. Kuanzia hapa chini inawezekana. Kuanzia kwa mwananchi inawezekana. Hawa watu wasitudanganye siku zote eti lazima tuongee mambo ya viongozi,” aliongeza Bw Ruto.
Kwenye mkutano huo, alimlaumu Rais kwa kuyumbisha Ajenda Nne Kuu za serikali ya Jubilee huku akiendeleza mchakato wa BBI. Akihutubu mjini Embu, Jumapili, Dkt Ruto alisema mpango huo unafaa kusitishwa kwa kuwa sio wa dharura kwa Wakenya. Hii ni tofauti na msimamo wa Rais Kenyatta kwamba, wakati umefika wa katiba kurekebishwa
Dkt Ruto alisema Rais Kenyatta alikoma kushughulika na ajenda za serikali na kuelekeza juhudi zake kufanikisha BBI. Alisema kwamba, mipango yote waliyokuwa nayo kwa nchi ililemazwa na kampeni za BBI.
“Sisi tulikuwa na mpango wa kitaifa wa makazi nafuu kama mojawapo ya Ajenda Nne Kuu ambao ulilenga kujenga nyumba 500,000 kila mwaka kote nchini, mpango huo ulikuwa wa kubuni nafasi za kazi kwa mafundi, maseramala, wahandisi, waashi na mafundi wa stima,” alisema Dkt Ruto.
“Lakini kazi hizo zilikosekana kwa sababu tumeambiwa kuna mradi muhimu zaidi unaoitwa BBI ambao unalenga kubuni nafasi nne au tatu za kazi kwa watu wachache,” alisema. Alisema ingawa walianza vyema kama serikali ya Jubilee, Rais Kenyatta alibadilisha ajenda walizokuwa nazo. Akiwa kaunti ya Meru Jumamosi, Dkt Ruto alimlaumu Rais Kenyatta kwa kukataa kampeni za mapema.
“Kuna wale ambao hawataki tuzungumzie mahitaji ya wananchi wa kawaida. Lakini hatutakoma. Lazima tubadilishe uongozi wetu uweze kujali watu wa mapato ya chini,” alisema.
Dkt Ruto alisema hayo muda mfupi baada ya Rais Kenyatta kusisitiza kuwa, mikutano ya kisiasa inagawanya Wakenya. Akihutubia viongozi wa bunge katika ikulu ya Nairobi, Rais aliwahimiza wanasisa kudhibiti azma zao ili kutoa nafasi kwa serikali kutumia kikamilifu utulivu kati yake na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga kustawisha taifa hili.
Lakini akiwa Igembe, Meru, Dkt Ruto alisema hatakoma kuendeleza kampeni yake ya kusaidia masikini kujiimarisha kimaisha kauli ambayo alirudia Jumapili akiwa Embu.
Septemba, Dkt Ruto aliongoza washirika wake katika mkutano kaunti ya Kajiado ambapo walidai usajili wa Wakenya kwa mfumo wa kidijitali, maarufu Huduma Namba unanuiwa kutumiwa kuiba kura zake kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
Mnamo Jumamosi, Rais Kenyatta ambaye amekuwa msitari wa mbele kuhakikisha usajili huo unafaulu aliwataka wanasiasa kutafuta ukweli kabla ya kutoa matamshi ya kupotosha umma. Kulingana na mdadisi wa siasa Joseph Katana, yamkini Dkt Ruto ameamua kumkabili Rais Kenyatta moja kwa moja katika hatua za kuhama Jubilee.