Siasa

Kampeni zafufua uhasama kati ya Joho na Mvurya

October 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MOHAMED AHMED

UHASAMA mpya umeibuka kati ya Gavana wa Kwale, Salim Mvurya na mwenzake wa Mombasa, Hassan Joho kuhusiana na uchaguzi mdogo wa Msambweni.

Bw Mvurya amemkemea Gavana Joho kwa kupeleka siasa za ubabe katika kaunti yake akisema kuwa, eneo hilo halitatumika kama uwanja wa vita.

“Mimi nimesikia mengi kutoka kwa wanasiasa wa ODM. Maneno mengine yalikuwa yanatoka kwa wenzangu magavana ambao wamesema watakuja kuweka kambi hapa. Lakini mimi nataka kuwaambia Kwale ni mahali pa heshima,” akasema Bw Mvurya.

Alisema Kwale si eneobunge, bali ni kaunti kamili yenye uongozi, hivyo basi viongozi ambao wameanzisha kampeni wanafaa wafanye kampeni hizo kwa heshima ya hali ya juu.

“Wale ambao wanataka kuweka kambi kwa sababu ya uchaguzi wa Msambweni ni wageni, lakini tunataka waendeshe kampeni kwa amani na wasitumie chama kugawanya wenyeji wa Kwale,” akaongeza.

Bw Mvurya alizungumza eneo la Bongwe/Gombato ambapo alitoa zabuni ya Sh1.7 milioni kwa wanafunzi wa vyuo vikuu Jumamosi, siku moja tu baada ya Gavana Joho kuongoza kundi la ODM kumpigia debe mgombeaji wao, Bw Omar Boga.

Bw Mvurya anamuunga mkono Bw Feisal Bader ambaye anaungwa mkono na Naibu Rais William Ruto.

Wakati alitua Kwale mnamo Ijumaa, Bw Joho alisema atamuonyesha Dkt Ruto kivumbi katika kinyang’anyiro hicho cha Msambweni.

“Kwanzia leo sisi tutakita kambi hapa. Mimi sitaondoka Msambweni. Mwanzo tutapangisha nyumba na tuishi hapa mpaka siku ya kura. Wataona kivumbi ambacho hawajawahi kuona maishani mwao,” akasema Bw Joho.

Bw Mvurya vile vile alisema hatakubali viongozi wakuu, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake Dkt Ruto na Bw Odinga kutukanwa kwa sababu ya kampeni hizo.

“Sisi tunaweheshimu viongozi hao watatu kwa sababu wote wana mchango katika maendeleo ya Kaunti ya Kwale. Kwale ni ya watu wa heshima na si mahali pa kufanya siasa za ubabe,” akaongeza.

Aliwasihi wakazi wa Kwale wasikubali kugawanywa kwa misingi ya vyama akiwaeleza kuwa siasa zitakuja na kwisha.

Alisema kuna haja ya wakazi kutekeleza maamumizi yaliyo na busara ifikapo Desemba 15 watakapopigia kura kiongozi wanayemtaka.

Juma lililopita, Bw Mvurya, alijitokeza wazi na kuwaomba wakazi hao wampigie kura Bw Bader akisema ndiye kiongozi anayewafaa.

Uchaguzi huo mdogo umesalia kuwa kati ya washindani wawili ambao ni Bw Boga na Bw Bader.

Wawili hao wanapojikakamua kuwania kiti hicho cha ubunge, Bw Boga ameweka matumaini yake kwa wapiga kura 17, 538 katika wadi ya Bongwe/Gombato ambapo alihudumu kama diwani huku Bw Bader akitegemea zaidi wadi za Ramisi (kura 18,569) na Ukunda 21,500.

Wadadisi wa kisiasa wamesema Bw Boga pia anatarajiwa kupata idadi nzuri ya kura katika wadi ya Ukunda. Bw Bader analenga wadi ya Ukunda kwa sababu baadhi ya watu wa familia yake wanaishi uko.

Taifa Leo pia imedokezwa kuwa Bw Boga anategemea uungwaji mkono wa Diwani wa Ukunda, Omar Kitengelee ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM pamoja na naibu mwenyekiti wa chama hicho tawi la Kwale, Bw Nicholas Zani. Bw Zani alishindwa katika mchujo wa chama.