• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Mawimbi makali ya Jubilee, Ruto, Miguna na NASA yamgonga Raila

Mawimbi makali ya Jubilee, Ruto, Miguna na NASA yamgonga Raila

Na WAANDISHI WETU

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga anakabiliwa na mawimbi makali ya kisiasa kutoka pande tofauti.

Hii ni baada ya aliokuwa akishindana nao kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, Jubilee, na pia waliokuwa washirika wake wakati huo katika NASA kumwelekezea makombora ya kila aina.

Anaporejea nyumbani Jumatano, wafuasi wake na wapinzani wako macho kuona jinsi atakavyokabiliana na mashambulizi kutoka kwa Naibu Rais William Ruto, waliokuwa washirika wake katika Muungano wa NASA, hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kutofautiana naye kuhusu marekebisho ya Katiba na cheche anazorushiwa na Miguna Miguna.

Bw Odinga aliondoka nchini kuelekea Uingereza wiki iliyopita akionekana kufurahia matunda ya mwafaka wake na Rais Kenyatta, lakini punde tu baada ya kuondoka, Rais alijitenga na mjadala wa kura ya maamuzi ya kubadilisha Katiba naye naibu wake akaanza kumshambulia.

Akihutubia wanachama wa sekta ya kibinafsi katika Ikulu ya Nairobi mwishoni mwa wiki, Rais Kenyatta alisema hana wakati wa kuzunguka nchini kupiga kampeni ya kura ya maamuzi.

Kabla ya kuondoka nchini, Raila alikuwa amezidisha mjadala wa kura ya maamuzi ili kubuni wadhifa wa waziri mkuu na viwango vitatu vya utawala, ambao umepingwa vikali na Bw Ruto.

Punde tu baada ya Rais Kenyatta kujitenga na mjadala huo, Bw Ruto alianzisha mashambulio dhidi ya Bw Odinga akimtaja kama dikteta na asiyekubali kushindwa. Matamshi hayo ya Bw Ruto akiwa Kaunti ya Nandi mwishoni mwa wiki yalizua malumbano kati ya wabunge wa ODM na Jubilee kila upande ukitetea kiongozi wao.

Malumbano hayo yalikuwa makali hivi kwamba baadhi ya wabunge wa Jubilee walipendekeza kudhamini mswada wa kuzuia watu waliofikisha miaka 70 kugombea urais wakimlenga Bw Odinga wanayedai anapanga kushiriki uchaguzi wa 2022.

Bw Ruto alikasirishwa na matamshi ya Raila akiwa London kwamba alishinda uchaguzi wa urais wa mwaka jana na kutilia shaka kujitolea kwake kufanikisha mwafaka wake na Rais Kenyatta.

Jumanne, akiwa Mombasa, Bw Ruto aliendeleza mashambulizi yake akisema wanaoitisha marekebisho ya Katiba ni wazembe ambao hawawezi kushinda uchaguzi wowote na wasio na maono ya maendeleo ya nchi.

“Nitasema tu kwamba wakati mwingine watu wavivu ambao hawataki kutia bidii na wasioweza kuunda sera za maendeleo hutumia Katiba kama kisingizio. Lakini sitaki tuzungumzie hilo hapa leo,” alisema Bw Ruto.

Mwingine aliyevuruga bahari ya kisiasa kwa Bw Odinga ni wakili Miguna Miguna aliyemtaja waziri huyo mkuu wa zamani kama mnafiki aliyesahau malengo yake ya kisiasa na kumezwa na Jubilee.

Mawimbi ya kisiasa yalizidi kumgonga Bw Odinga baada ya mwenyekiti wa chama cha Wiper, Kivutha Kibwana, kumshauri Kalonzo Musyoka kujitenga na Bw Odinga na kuanza mwelekeo mpya wa kisiasa, ishara kwamba itakuwa vigumu kunusuru muungano wa NASA.

 

Na BENSON MATHEKA, MOHAMED AHMED, IBRAHIM ORUKO na VALENTINE OBARA

 

You can share this post!

Madiwani wasisitiza kupewa magari ya kifahari na pensheni

Weita mpenda ombaomba amwaga unga

adminleo