• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
WANDERI: Waafrika wangali watumwa wa Wazungu

WANDERI: Waafrika wangali watumwa wa Wazungu

Na WANDERI KAMAU

BAADA ya nchi za Afrika kujinyakulia uhuru wao kutoka kwa wakoloni katika miaka ya sitini, tumaini kuu la kila mmoja lilikuwa kwamba huo ulikuwa mwanzo mpya.

Hata hivyo, kilicho wazi ni kwamba Mwafrika ni yule yule. Angali anawaabudu Wazungu. Inawezekana waliondoka humu, ila ukweli ni kwamba kidhana wangali watumwa wao.

Hili lilidhihirika Jumamosi iliyopita, wakati dunia nzima ilitekwa na msisimko wa “harusi ya kifalme” kati ya Mwanamfalme Harry na mwanadada Meghan Markle.

Vyombo vya habari vilitenga makumi ya kurasa kuangazia “upekee” wa harusi hiyo. Redio na runinga barani Afrika ziliahirisha baadhi ya vipindi muhimu ili kutoa nafasi kwa “matangazo ya moja kwa moja” ya harusi hiyo.

Magazeti hayakuachwa nyuma, kwani yalikosa kuchapisha baadhi ya habari muhimu zinazowaathiri wasomaji wake, ili “kutoa nafasi ya kutosha kwa harusi hiyo.”

Hayo tisa, kumi ni kwamba, kuna hoteli iliyowatoza Wakenya waliotaka kuifuatilia harusi hiyo “vizuri” Sh1 milioni!

Hii ndiyo ishara kwamba hatuogelei tu katika maruerue ya ukoloni mamboleo, ila tushakubali kwa nafsi zetu kwamba tu watumwa.

Kuna maswali kadhaa: Ni umuhimu gani raia walipata kwa kuahirisha baadhi ya shughuli muhimu ili kufuatilia harusi hiyo? ‘Upekee’ wake una manufaa gani kwa Mwafrika?

Ni hasara ipi ambayo vyombo vya habari vingepata ikiwa vingeangazia masuala muhimu yanayoziathiri nchi zao badala ya kuipa kipao mbele hafla isiyo na manufaa yoyote kwao? Ni manufaa yapi ambayo waliooana walipata kwa kuangaziwa na vyombo vya habari vya Kiafrika au nchi zinazostawi kiviwanda?

Ni mkasa kwamba katika karne ya 21, utamkuta Mwafrika akishabikia kandanda ya Uingereza, Uhispania na kwingineko, wakati akiwa hafahamu lolote kuhusu yanayojiri katika nchi yake.

Kulingana na msomi Francis Fukuyama, kwenye kitabu ‘The End of History’ (Mwisho wa Historia) mkasa mkuu katika maisha ya binadamu ni kudhibitiwa kidhana na mwingine bila ufahamu wake.

Vile vile, anaonya kwamba ukoloni mbaya zaidi ni ule unaohusu ‘vita’ dhidi ya tamaduni na mitindo ya kimaisha ya jamii husika, vile wanavyofanya Wazungu dhidi ya Waafrika.

Hivyo, wajibu mkuu kupigana vita hivi ni wazazi wa kizazi cha sasa kufahamu kwamba watabaki kuwa watumwa wa Kizungu ikiwa hawatazinduka.

[email protected]

 

You can share this post!

TAHARIRI: IPOA ilikosa kuafikia matarajio ya wengi

Majambazi waitisha matiti 540 ya wanawake

adminleo