Walimu wakuu sasa wapinga wanafunzi wote kurejea shuleni
Na CHARLES WASONGA
WALIMU wakuu wa shule za upili sasa wanapinga mpango wa serikali wa kuwaagiza wanafunzi wengine kurejelea masomo wakisema, taasisi hizo haziwezi kumudu idadi kubwa ya wanafunzi.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu hao (KESSHA) Kahi Indimuli alisema Jumatatu, shule hizo hazitaweza kuzingatia kanuni ya Wizara ya Afya za kuzuia maambukizi ya corona, haswa umbali wa mita moja kati ya wanafunzi.
Kulingana na Bw Indumuli hiyo inachangiwa na hali kwamba tangu kufungwa kwa shule baada ya kuzuka kwa mlipuko wa janga la corona nchini, shule hazijaweza kuongeza madarasi zaidi.
“Tutakabiliwa na wakati mgumu iwapo leo Waziri wa Elimu atatangaza kwamba, wanafunzi wote warejee shuleni ikizingatiwa kuwa idadi ya maambukizi imekuwa ikiongezeka. Msongamano utashuhudiwa shuleni haswa katika shule za mabweni kwa sababu hatuna madarasa na mabweni zaidi,” Bw Indimuli akasema Jumatatu asubuhi kwenye mahojiano katika Redio Citizen. Duru kutoka Wizara ya Elimu zinasema huenda wanafunzi wengine wakaagizwa kurejea shuleni kuanzia Oktoba 26, 2020.
Bw Indimuli ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Machakos, alisema japo baadhi ya shule za upili zilikuwa zikijenga madarasa zaidi kabla ya kuzuka kwa corona, mpango huo hautafaa katika hali ya sasa.
“Chini ya mpango huo, darasa moja lilistahili kuhudumia wanafunzi 50 lakini sasa kila darasa litahitaji wanafunzi 25, jambo ambalo haliwezekani wakati huu,” akasema.
Bw Indimuli aliongeza kuwa, walimu wakuu wameingiwa na hofu kwamba, endapo wanafunzi wa vidato vya kwanza hadi tatu watarejea shuleni, hatua hiyo itahatarisha maisha ya wanafunzi wa kidato cha nne, “ikizingatiwa kuwa maambukizi ya corona yameongezeka tangu kufunguliwa kwa shule hizo.”
Tangu Oktoba 5, wanafunzi wa Gredi 4, Darasa la 8 na Kidato cha 4 waliporejea shuleni, Kenya imekuwa ikiandikisha visa 600 vya maambukizi, kwa wastani.
Hii ina maana kuwa, kiwango cha maambukizi kimepanda hadi asilimia 12 kutoka asilimia nne Septemba serikali ilipolegeza zaidi masharti ya kuzuia maambukizi ya Covid-19.