WASONGA: Anayopinga Ruto katika BBI huenda yamfae hata zaidi
Na CHARLES WASONGA
NAIBU Rais William Ruto amekuwa mstari wa mbele kupinga mabadiliko ya Katiba yanayopendekeza kubuniwa kwa nyadhifa zaidi za uongozi akisema haja yake kuu ni kuanzisha utawala unaojali masihali ya masikini.
Dkt Ruto anapinga kubuniwa kwa nyadhifa za Waziri Mkuu na manaibu wake wawili, pamoja na wadhifa wa kiongozi wa rasmi wa upinzani, ambao utamwendea atakayeshikilia nafasi ya pili katika kinyang’anyiro cha urais.
Akiongea juzi katika kaunti ya Meru, alidai mabadiliko hayo yanayobashiriwa kupendekezwa kweye ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) yanalenga kutoa “nafasi za ajira kwa watu wanne pekee”.
Ningependa kumshauri Naibu Rais kwamba endapo ni kweli anataka kuingia Ikulu 2022, pendekezo hilo la kupanuliwa kwa kitengo cha uongozi litamfaa zaidi.
Nyadhifa hizo zitamsaidia “kutongoza” uungwaji mkono kutoka kwa wanasiasa kutoka sehemu mbalimbali nchini, kwa kuwaning’inizia nyadhifa hizo kila anapozuru maeneo mbalimbali nchini. Huo ndio umekuwa mti wa wawaniaji urais tangu taifa hili liliporejelea utawala wa vyama vingi mnamo 1992.
Tayari Dkt Ruto amefaulu kupata washirika kutoka takriban maeneo yote ya nchini. Atahitaji kuahidi wafuasi wake kutoka maeneo hayo nyadhifa katika serikali yake atakayounda kwani masilahi ya kibinafsi ndiyo huendesha siasa za taifa na mataifa mengine katika mataifa ya Afrika.
Hii ina maana kuwa atalazimika kubuni muungano wa kisiasa ambayo utashirikisha vyama, vuguvugu kutoka pembe zote za nchini kwani dalili iko wazi kwamba hatawania urais kwa tiketi ya Jubilee.
Ni siri iliyo wazi kuwa wapinzani wa Dkt Ruto, mrengo wa kiongozi wa ODM Raila Odinga na wandani wa Rais Kenyatta kutoka Mlima Kenya, wanapanga kuunda muungano wa kisiasa watakaoutumia kuzima ndoto yake (Ruto) ya kuingia Ikulu. Hii ndio maana wanaunga mkono mageuzi ya Katiba kupitia kura ya maamuzi kwa ajili ya kupanua kitengo cha uongozi.
Rais Uhuru Kenyatta wiki jana alikariri kuwa mageuzi ya Katiba ndiyo “njia ya kipekee ya kuzima uwezekano wa taifa hili kutumbukia katika machafuko ya kisiasa ilivyoshuhudiwa katika chaguzi zilizopita.”
Hii ina maana kuwa endapo Dkt Ruto atadiriki kupinga BBI, ataendelea kutengwa zaidi serikalini hali ambayo itamfanya kuwania urais 2022 “kama mwaniaji wa upinzani.”
Akome kuwadanganya Wakenya kuwa serikali yake itakuwa ya walalahoi, maarufu kama mahasla huku ile ya wakereketwa wa BBI itakuwa ya matajiri.
Ukweli ni kwamba wanasiasa wandani wa Dkt Ruto ndio watashikilia nyadhifa kuu katika serikali yake, endapo atashinda urais.
Akina mama mboga, waendeshaji bodaboda, wasusi, makondakta wa matatu na raia wengine wa tabaka la chini hawatapata chochote. Kazi yao itakuwa kupiga kura 2022 kisha warejelee maisha yao ya kawaida kama mahasla.