KAMAU: Viongozi wa bara Afrika wamewasaliti mashujaa
Na WANDERI KAMAU
IKIWA wangefufuka leo, huenda hawangetusamehe hata kidogo.
Nawazungumzia viongozi walioweka msingi kwenye utetezi na ukombozi wa Afrika kama Julius Nyerere (Tanzania), Dedan Kimathi (Kenya), Kwameh Nkrumah (Ghana), Nelson Mandela (Afrika Kusini) miongoni mwa wengine.
Waliposhiriki kwenye harakati hizo, lengo lao lilikuwa kuona bara lililojisimamia kisiasa, kiuchumi na kitamaduni—bila mwingilio wa aina yoyote wa kigeni.
Ni kwa imani hiyo ambapo walifanya kila wawezalo kuondoa tawala za kikoloni barani humu.
Hapa nchini, Shujaa Dedan Kimathi aliwaongoza wapiganiaji wa Maumau dhidi ya utawala wa Waingereza katika misitu ya Aberdare na Mlima Kenya.
Ghadhabu ya Kimathi ilitokana na hatua ya walowezi wa Kizungu kunyakua mashamba ya Waafrika na kuyafanya yao bila ruhusa kutoka kwao.
Ingawa hawakuwa na silaha hatari kama Wazungu, wapiganaji waliungana na kuzingatia mwito wa viongozi wao kumkabili Mzungu bila kumwogopa.
Vita hivyo vilidumu kati ya 1952 na 1960. Kukamilika kwake kulijenga matumaini mapya miongoni mwa wale walioshiriki kuwa hatimaye harakati zao zingezaa matunda.
Waliamini kwamba umwagikaji damu ambao walipitia waliposhiriki kwenye vita hivyo ungegeuka kuwa baraka kwao na vizazi vyao.
Hata hivyo, Usaliti Mkuu ulianza pale viongozi Weusi walipochukua uongozi wa mataifa hayo.
Hapa Kenya, kiongozi yeyote aliyepaaza sauti yake kuwatetea wanyonge alikumbana na “ukali kamili” wa serikali iliyokuwepo.
Mtindo huo ndio ‘uliwanyamazisha’ watu kama Pio Gama Pinto, Tom Mboya, JM Kariuki kati ya wengine.
Waliuawa kwa kuonekana kama “wasumbufu” kwa serikali na utawala uliofuata.
Mkondo huo ndio ulishuhudiwa katika nchi zingine za Afrika. Watetezi halisi wa ukombozi walitengwa, kunyamazishwa na kudhalilishwa kwa kila njia.
Ndivyo hali ilivyo hadi sasa. Swali ni: Ikiwa wangefufuka leo, mashujaa hao wangefurahia hali zilizo katika nchi nyingi za Afrika? Wangependezwa na hali za kiuchumi na mazingira ya kisiasa yaliyo katika nchi hizo? Wangefurahia ‘matunda’ ya umwagikaji damu uliotokea waliposhiriki kwenye harakati za ukombozi?
Imani yangu ni kuwa wangekasirishwa na kutamaushwa na hali ilivyo. Hawangetusamehe. Pengine wangejutia harakati zao na kumwambia Mungu kuwarejesha kwenye ulimwengu wa wafu. Hawangetamani hata kidogo kuishi duniani.
Sababu kuu ni kuwa viongozi waliotwikwa jukumu la kuendeleza ndoto zao walizisaliti. Hapa Kenya, watu maskini wanaendelea kunyanyaswa kila kuchao kwa kisingizio cha ‘maendeleo.’
Vibanda vya watu maskini vinabomolewa kote kote. Biashara zao zinamalizwa kwa kisingizio cha kuwa ‘ngome’ za uhalifu, huku wanao wakilazimika kuishi kama maskwota katika nchi yao yenyewe.
Vilio vya wanyonge vimekuwa kama ‘usumbufu’ kwa mabwanyenye na wanasiasa wanaoendesha udhalimu huo.
Naam, Nchi ya Matumaini imegeuka kuwa Taifa la Majonzi na Dhuluma. Vijana wanaishi leo wasijue la kesho kutokana na ukosefu wa ajira. Tu nchi ya laana, mashaka na usaliti.
Nchi ya watu wala watu; binadamu waliopoteza utu na hali ya kujaliana. Kwa wasiojua, maasi ya umma huanzia hivi. Tunahitaji mwanzo mpya!