Michezo

AK yalenga kutafuta suluhu dhidi ya matumizi ya pufya

October 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

MWENYEKITI wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) Tawi la Nairobi, Barnaba Korir amewataka wanariadha wa Kenya kuongoza shughuli za uhamasishaji katika sehemu zote za humu nchini kuhusu umuhimu wa kuepuka matumizi ya dawa za kusisimua misuli michezoni.

Rai ya Korir inatolewa siku chache baada ya mwanariadha Daniel Wanjiru aliyeibuka bingwa wa London Marathon mnamo 2017, kupigwa marufuku ya miaka minne kwa hatia ya kutumia dawa haramu za kusisimua misuli.

Pendekezo hilo limeungwa mkono na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia katika marathon, Patrick Makau ambaye amesisitiza kwamba Kenya iko katika hatari ya kupigwa marufuku kwenye ulingo wa riadha iwapo visa vya matumizi ya pufya miongoni mwa wanariadha vitakithiri.

“Tunalenga sana kuhifadhi hadhi ya taifa letu. Kenya ni ngome ya wanariadha wa haiba kubwa ambao wamekuwa wakitikisa ulimwengu kila mwaka kwa mafanikio yao ya kutamanisha bila kutumia dawa. Hivyo, hatutaki jina la Kenya lipakwe tope zaidi ulimwenguni kwa sababu ya watu wachache wabinafsi wanaopania kutumia njia za mkato kujitafutia ufanisi,” akashikilia Korir.

Kwa upande wake, Waziri wa Michezo, Amina Mohamed amesema Serikali inapangia kupitisha sheria itakayoshuhudia wanamichezo wanaotumia dawa za kusisimua misuli wakiadhibiwa vikali kwa kiwango sawa na wahalifu wengine wanaofungwa jela kwa makosa ya jinai.

Kitengo cha Maadili (AIU) cha Shirikisho la Riadha Duniani (WA) kilikuwa kimempiga Wanjiru marufuku ya muda mnamo Aprili 14 mwaka huu baada ya hitilafu kubainika kwenye rekodi zake za vipimo vya afya.

Kwa mujibu wa Jopo la Nidhamu la WA, adhabu kwa Wanjiru, 28, inaanza kutekelezwa kuanzia Disemba 9, 2019 na matokeo yote aliyoyasajili kuanzia Machi 2019 yamefutiliwa mbali.

Kati ya matokeo hayo ni ushindi wa nishani ya shaba aliojinyakulia kwenye Vitality Big Half Marathon jijini London mnamo Machi 2020. Wanjiru aliwahi pia kuambulia nafasi ya 11 kwenye London Half Marathon mnamo Aprili kabla ya kuibuka wa 11 kwenye mashindano ya Kenya Police mnamo Julai mwaka huu.

Wanjiru alijipa umaarufu mnamo 2017 alipombwaga Mwethiopia Kenenisa Bekele kwenye London Marathon kabla ya kutupwa nafasi ya nane kwenye Riadha za Dunia zilizoandaliwa London, Uingereza mnamo 2017.

Jumla ya sampuli 16 za damu ya Wanjiru zilifanyiwa vipimo kati ya Aprili 20, 2017 na Aprili 29, 2019. Sampuli ya 14 ya damu yake ilichukuliwa mnamo Machi 9, 2019, siku moja kabla ya kufunga safari ya kuelekea London.

Alishiriki mbio za London Half Marathon (Vitality Big Half) mnamo Machi 10, 2019 kabla ya kurejea humu nchini mnamo Machi 11, 2019 na sampuli ya 15 ya damu yake kuchukuliwa Machi 13, 2019.

Sampuli hizo zilitathminiwa na wataalamu watatu wa pufya – Dkt Laura Garvican Lewis, Prof Giuseppe d’Onofrio na Dkt Paulo Paixao – ambao walibaini uwepo wa chembechembe nyingi za dawa haramu za kusisimua misuli katika sampuli ya 14 ya damu ya Wanjiru.

Jumla ya Wakenya tisa wamepigwa marufuku na WA chini ya kipindi cha miezi minne iliyopita kwa hatia ya kushiriki pufya. Wawili kati yao ni washindi wa zamani wa London Marathon.

Wilson Kipsang aliyeibuka mshindi wa London Marathon mnamo 2012 na 2014 alipigwa marufuku ya miaka minne mnamo Juni kwa kukosa kujiwasilisha kufanyiwa vipimo vya afya na kutoa ushahidi wa uongo wakati wa kujitetea.

Wajiru anaadhibiwa wiki tatu pekee baada ya Patrick Siele, aliyeibuka katika nafasi ya 12 kwenye Venloop Half Marathon nchini Uholanzi na nafasi ya tisa kwenye Cardiff Half Marathon nchini Uingereza mwaka jana, kupigwa marufuku ya miaka mitatu na wiki sita.

Mkenya mwingine wa mbio za masafa marefu, Philip Kangogo alipigwa marufuku ya miaka miwili kwa kukiuka kanuni za WA zinazodhibiti matumizi ya pufya.

Siele na Kangogo sasa wanaunga orodha ya wanariadha wa humu nchini ambao wamepigwa marufuku ya kati ya miaka miwili na minane kwa hatia ya kukosa kujiwasilisha kufanyiwa vipimo vya afya au kutumia pufya kama njia ya mkato ya kujitafutia ufanisi kwenye riadha.

Mercy Kibarus alipigwa marufuku ya miaka minane kuanzia Septemba 2019 kwa kutumia pufya huku Kenneth Kipkemoi na Alex Korio Oliotiptip wakipokezwa miaka miwili kila mmoja kwa kutumia dawa haramu za kusisimua misuli na kukosa kujitokeza kupimwa mara tatu ili kubaini iwapo aliwahi kutumia pufya mtawalia.

Mikel Kiprotich Mutai, Vincent Kipsegechi Yator na Peter Kwemoi walipigwa marufuku ya miaka minne kila mmoja kwa kutumia pufya. Bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500 mnamo 2017 Elijah Manang’oi, James Kibet na Alfred Kipketer aliyeibuka bingwa wa dunia katika mbio za mita 800 kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, wanafanyiwa uchunguzi baada ya kupigwa marufuku ya muda.

Kwa mujibu wa kanuni za Shirika la Kukabiliana na Pufya Duniani (WADA), mwanariadha anayekosa kufanyiwa vipimo mara tatu chini ya kipindi cha miezi 12, hupigwa marufuku moja kwa moja.

Kenya iko katika kategoria ya kwanza (A) ya mataifa ambayo wanamichezo wao wanatumia sana dawa haramu ili kujipatia ufanisi kwa njia za mkato. Nigeria, Ethiopia, Bahrain, Morocco, Ukraine na Belarus ni mataifa mengine katika kategoria hiyo.

Kenya imekuwa ikimulikwa sana na shirika la kupambana na pufya duniani (WADA) pamoja na IAAF kutokana na kukithiri kwa visa vya matumizi ya pufya miongoni mwa wanariadha wake tangu 2012. Tangu mwaka huo, zaidi ya watimkaji 40 wamepigwa marufuku. WADA imefichua kuwa wanariadha 138 kutoka Kenya wamewahi kutumia pufya kati ya 2004 na Agosti 2018.