Beki Washington Munene atia saini mkataba wa miaka miwili kambini mwa AFC Leopards
Na CHRIS ADUNGO
AFC Leopards wamempokeza beki Washington Munene mkataba mpya wa miaka miwili.
Nyota huyo wa zamani wa Nairobi Stima aliingia kambini mwa Leopards mwanzoni mwa msimu wa 2019-20 baada ya kuagana na Wazito FC kwa mkopo.
“Tumeafikiana na Munene kwamba atajiunga sasa na Leopards kwa mkataba wa kudumu. Alijiunga nasi mnamo Septemba 2019 kutoka Wazito. Aliridhisha sana uwanjani ndiposa usimamizi umekuwa mwepesi wa kurefusha kipindi cha kuhudumu kwake nasi,” ikasema taarifa ya Leopards ambao ni mabingwa mara 13 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL).
Munene anakuwa mchezaji wa tatu baada ya kiungo Collins Sichenje na kipa raia wa Uganda, Benjamin Ochan kurefusha mkataba wake kambini mwa Ingwe.
Leopards ambao ni mabingwa mara 13 wa Ligi Kuu ya Kenya kwa sasa wanashiriki mazungumzo na fowadi Elvis Rupia kuhusu uwezekano wa kutia saini mkataba mpya baada ya kandarasi yake ya awali kutamatika Aprili 2020.
Hata hivyo, Rupia amefichua azma ya kutia saini mkataba mfupi na Leopards kwa kuwa maazimio yake ni kuingia tena katika sajili rasmi ya kikosi cha ughaibuni. Kabla ya kusajiliwa na Wazito FC mnamo 2019, Rupia alikuwa amehudumu kambini mwa Power Dynamos nchini Zambia.
“Ingwe wamekuwa wazuri kwangu licha ya kwamba mkataba wangu nao ulitamatika Aprili. Itakuwa vyema iwapo nitarejesha hisani walionitendea kwa kurefusha zaidi kipindi changu cha kuhudumu nao japo kwa muda mfupi ujao,” akasema Rupia.
Leopards wanatarajiwa wiki hii kutambulisha rasmi wanasoka wapya walioingia kambini mwao muhula huu kwa mashabiki.