MATHEKA: Walio mamlakani wakome kuwatumia polisi visivyo
Na BENSON MATHEKA
MIKUTANO ya Naibu Rais William Ruto Kaunti ya Nyamira, Meru na Embu mwishoni mwa wiki imedhihirisha kuwa maafisa wa polisi wanaweza kutekeleza kazi yao bila kutumia nguvu kupitia kiasi wakipatiwa maagizo yanayofaa.
Mikutano hiyo haikukumbwa na vurugu na polisi walifanya kazi yao ya kudumisha usalama. Hii ilikuwa tofauti sana na walipovunja mikutano ya awali ya washirika wa Naibu Rais kaunti ya Kakamega kwa kuwarushia gesi ya kutoa machozi.
Hii imekuwa kawaida ya polisi kila wakati raia wanapotekeleza haki yao ya kuandamana kwa amani. Wamekuwa wakivunja maandamano ya amani, kuwapiga watu na kuwakamata hata wakati wamewafahamisha kuhusu nia yao ya kuandamana. Baadhi ya watu wameuawa au kulemazwa kabisa kwa kupigwa na maafisa wa polisi bila hatia yoyote.
Wanaowapa maagizo ya kufanya hivi huwa wanawafanya polisi kuonekana kama maadui wa raia ilhali kulingana na katiba, maafisa wa usalama wanafaa kuwa marafiki wa wananchi. Vitendo vya ghasia wakati polisi wanapovunja mikutano ya amani vimesawiri Kenya kuwa nchi ya fujo. Hii inaweza kuwatia hofu wawezekezaji wa kimataifa ambao mchango wao ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wetu.
Hivyo basi, mtindo huu wa kuwapa maagizo maafisa wa usalama kutumia nguvu kupita kiasi unafaa kukomeshwa ikiwa Kenya itaheshimiwa kama nchi inayotambua na kulinda katiba yake na haki za raia wake.
Katiba inayotoa haki ya usalama kwa wote, katiba inayohakikishia kila mtu haki na uhuru wa kujieleza, kukusanyika na kutangamana haifai kupakwa tope na maagizo ya maafisa wachache wanaotaka kulinda maslahi ya kibinafsi.
Hata hivyo, uhuru huu una mipaka yake na inapovukwa, polisi wako na haki ya kutumia nguvu kiasi, sio kupita kiasi, mbali kurekebisha hali kwa kutumia mbinu walizofunzwa.
Maafisa wa polisi wakitumiwa vyema, uhusiano wao na raia utaimarika. Sio kila wakati wanafaa kulaumiwa kwa kutumia nguvu kwa sababu kuna nyakati wanapolazimika kuchukua hatua kujikinga. Tumeona mara kadhaa raia wakiwarushia mawe, tumeona baadhi ya watu wakivunja maduka wakati wa maandamano. Tumeona watu wakilipa vijana kukakabili waandamanaji wanaolalamikia hatua wanazounga mkono. Hali kama hii inapotokea, polisi hawafai kulaumiwa wanapotumia nguvu kutawanya au kukataa kuidhinisha mikutano ya kisiasa na maandamano.
Kuepuka makabiliano ya raia na polisi, kila mmoja anafaa kuheshimu sheria bila kujali cheo na tabaka lake. Walio mamlakani wanafaa kukoma kutumia polisi kuhangaisha wapinzani wao nao polisi wanafaa kutekeleza majukumu yao bila ubaguzi.
Sio siri kwamba polisi wamekuwa wakinyima baadhi ya wanasiasa vibali vya kuandaa mikutano huku wakiwaruhusu wengine. Hii haimaanishi polisi wasitelekeze majukumu yao ya kudumisha usalama kwa kukabiliana na wahalifu. Hii haimaanishi wasiheshimu wakubwa wao. Nao wakubwa wao hawafai kuwapa maagizo yaliyo kinyume cha katiba.
Wanasiasa nao wanafaa kuwa mfano mwema kwa kutambua umuhimu wa polisi na kuwaheshimu. Uhusiano mwema wa polisi na raia ni muhimu kwa usalama wa nchi.