• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
WANGARI: Vyuo viendelee kudhihirisha uwezo wao kiteknolojia

WANGARI: Vyuo viendelee kudhihirisha uwezo wao kiteknolojia

Na MARY WANGARI

HUKU shughuli za ufunguzi wa taasisi za elimu zikiendelea nchini, pana haja ya kuwepo mwamko mpya kwa vyuo vikuu nchini.

Licha ya kupitia makali ya janga la corona sawa na sekta nyinginezo nchini, taasisi za elimu ya juu nchini zimeweza kumudu hali na hata kuendeleza wajibu wake katika tasnia mbalimbali.

Katika kipindi cha miezi saba pekee tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kiripotiwe nchini mnamo Machi mwaka huu, vyuo vikuu vimejitokeza kwa ukakamavu na kuthibitisha nafasi yake katika jamii,

Ni bayana kuwa wajibu wa taasisi za juu za elimu katika kuendeleza sayansi na teknolojia kupitia tafiti na uvumbuzi anuai haujawahi kudhihirika vyema zaidi kushinda mwaka huu.

Mwaka wa 2020 bila shaka utakumbukwa kama mwaka ambao vyuo vikuu vilishuhudiwa vikishirikiana na serikali kuunda vifaa vya kupambana na janga hili la kiafya lililolemaza mifumo ya kiuchumi kote duniani.

Kuanzia kutengeneza vifaa vya kujikinga na gonjwa hilo kama vile barakoa, dawa za kuua viiini, vifaa vya kuwasaidia wahasiriwa kupumua katika vitengo vya wagonjwa mahututi hadi vitanda vya kutumika katika wadi hospitalini.

Ni baadhi tu ya mambo yaliyofanikishwa na vyuo vikuu nchini kwa ushirikiano na serikali katika viwango mbalimbali.

Isitoshe, taasisi za elimu ya juu nchini, licha ya kukabiliwa na athari hasi za kiuchumi, zimemudu kuimarisha mfumo wa masomo kimtandao.

Kupitia mfumo huo, vyuo vikuu nchini vya kininafsi na vya umma vimeweza kuwasajili wanafunzi, kuendeleza masomo, kuwalipa wakufunzi mishahara yao na hata kufanikisha hafla ya kufuzu kwa maelfu ya mahafala mitandaoni.

Ikiwa kuna kipindi ambapo taasisi za elimu nchini zimewekwa kwenye mizani kubainisha iwapo kweli zinastahili nafasi yake kama fahari ya jamii, basi ni hiki na kwa vyovyote vile ni bayana kuwa baadhi ya vyuo vikuu, endapo si vyote vimehitimu.

Huku hali ikionekana kurejea kawaida, vyuo vikuu viwe vya kibinafsi au vya umma havipaswi kulegeza kamba.

Ni sharti viendelee kupiga hatua kupitia uvumbuzi na utafiti na kusuluhisha matatizo tele yanayokabili taasisi hizo na jamii kwa jumla.

Ulimwengu unaporejelea taratibu hali ya kawaida, ni sharti vyuo vikuu nchini viimarishe mfumo wa masomo kidijitali ambao una nafasi muhimu hasa katika karne na enzi hii ya maendeleo kisayansi na kiteknolojia.

Isitoshe, wakati umewadia kwa vyuo vikuu nchini kuimarisha nafasi yake kwa kutekeleza wajibu wake katika jamii kupitia maarifa na tafiti mbalimbali.

Ni kwa kutumia maarifa yake kielimu na kusuluhisha matatizo anuai yanayokabili wanajamii ndipo tu vyuo vikuu vitavutia tena imani ya wanajamii na kujitokeza tena kama taasisi za kujivunia.

[email protected]

You can share this post!

MATHEKA: Walio mamlakani wakome kuwatumia polisi visivyo

Huu ndio wakati wa BBI – Uhuru