KINA CHA FIKIRA: Adui ni sumu kali, ukimficha kwako basi atakudhuru!
Na WALLAH BIN WALLAH
ADUI ni mtu au mnyama au kiumbe chochote kinachoweza kukutendea maovu!
Ukijua kuwa kiumbe fulani au mtu yeyote anaweza kukudhuru, umwogope na kumwepuka kabisa! Ukimwamini adui na kumkaribisha kwako, ni sawa na kukiingiza kichwa chako katika kinywa cha mamba mwenye njaa!
Adui si rafiki! Lakini watu wengine wana tabia za kuwaficha maadui badala ya kuwafichua kwa kuwa ni ndugu zao au jamaa ama wenzao! Kwa mfano shuleni, wakati mwingine wanafunzi wanamjua mwenzao ambaye huiba, huvuta bangi na kubugia dawa za kulevya, lakini humficha tu badala ya kuwadokezea walimu ili wachukue hatua mapema! Baadaye mwanafunzi huyo huyo aliyefichwa ndiye atakayeongoza mgomo shuleni na kusababisha mabweni kuchomwa moto na kuyavuruga masomo shuleni!
Pia nchini kwenye midani ya kisiasa, jamii ina mazoea ya kuwaficha wachochezi waenezao chuki za kikabila kutoka jamaa zao au ndugu zao ama rafiki zao. Utashangaa wanapomsifia mchochezi, “Huyu ndiye shujaa wetu!” Kwani hawajui kwamba mchuma janga hula na wa kwao? Mtu mwovu si rafiki! Usimfiche!
Siku moja Mama Tuka alienda shambani kulima. Alikuwa na mtoto wake mchanga aliyeitwa Tuka. Akamtandikia leso kwenye kivuli cha mti pale shambani. Akamlaza. Mtoto akalala fofofo! Mama akaanza kulima. Baada ya dakika arubaini hivi, Mama Tuka alisikia kelele kwa mbali, “Huyo! Huyo! Fisi huyo! Amewaua mbuzi wetu! Auawee!!!” Mara mama akamwona fisi akikimbia kuelekea pale shambani alipokuwa! Fisi alipofika alisimama akihema! Akamwambia mama, “Tafadhali unifiche! Wanataka kuniua bure bure! Unisaidie!”
Mama Tuka alimwambia fisi alale chini haraka! Akamfunika kwa nyasi na majani! Akachukua kitenge na sweta akaweka juu ya nyasi zilizomfunika fisi. Mama akaendelea kulima. Watu wale walipofika walimwuliza mama, “Mama, umemwona fisi amepitia hapa?” Mama Tuka alijibu kwa hasira, “Mimi sijamwona fisi! Sikuja hapa kumchunga fisi!” Wale watu walisema, “Mama, fisi ni adui! Usimfiche fisi! Usimfiche adui!” Wakaondoka!
Watu wale walipoenda kabisa, Mama Tuka alimfunua fisi akamwambia, “Ondoka uende! Adui zako wameenda!” Fisi alisema, “Siwezi kuenda hivi hivi tu! Nina njaa!” Mama alishtuka, akauliza, “Sasa unataka nikupe chakula gani?” Fisi alijibu kwa ukali, “Sitaki maswali yoyote! Nipe mtoto wako yule pale nimle sasa hivi!”
Fisi akamrukia mtoto Tuka akaanza kumla bila huruma! Mama alilia kwa uchungu lakini wapi! Aliyakumbuka maneno aliyoambiwa, “Mama, usimfiche adui! Fisi ni adui!”
Ndugu wapenzi, adui si rafiki! Ukimficha mwovu, atakudhuru! Adui ni sumu, utajiua mwenyewe!