Makala

Jinsi ya kujikinga dhidi ya kansa ya mapafu

October 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA WANGU KANURI

Kulingana na uratibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) saratani ya mapafu ndiyo inayoongoza kwa wagonjwa milioni 2.9 duniani. Isitoshe, saratani hii ndiyo inayoongoza kwa vifo kwa takwimu za milioni 1.76.

Licha ya kuwa kansa hii huwaathiri wanawake kwa wanaume, wanaume ni wengi ikilinganishwa na waathiriwa wanawake. Uvutaji wa sigara na tumbaku ndio sababu kuu ya kansa hii.

Hali kadhalika, mtu asiyevuta sigara ama tumbaku lakini anajihusisha na mtu anayevuta huwa na athari ya kuipata kansa hii ya mapafu.

Utaweza kufahamu kuwa unaugua saratani hii ya mapafu kwa kuwa na dalili hizi. Moja, kupunguka kwa uwezo wako wa kupumua. Hii ni kwa sababu saratani hii huzuia njia kuu za kupumua zilizoko kwenye mapafu.

Zaidi ya hayo, saratani hii inaweza sababisha majimaji kuwepo kwenye mapafu huku majimaji hayo yakizuia pafu iliyoathirika kupanuka vyema mtu akipumua.

Kukohoa damu hii kunatokana na kutokwa na damu kwenye njia ya kupumua. Kutokwa kwa damu kukiendelea kwa muda mrefu, mgonjwa hushauriwa kupokea matibabu ili kupunguza damu imtokayo akikohoa.

Mgonjwa wa saratani hii ya mapafu huwa na majimaji kwenye kifua chake. Majimaji haya hujaa katika nafasi inayozingira pafu lililoathirika na fukuo la kifua (chest cavity).

Kuwepo kwa majimaji haya kunaweza sababisha upungufu wa kupumua huku mgonjwa akishauriwa kupokea matibabu ili majimaji haya yaweze kutolewa.

Pia, huwa mwenye uchungu mwingi hata baada ya saratani hii kuenea. Tanbahi kuwa pindi saratani ya mapafu imeenea zaidi ya mapafu, ni vigumu mno mgonjwa kupona. Kunayo matibabu ya kupunguza makali ya kansa ili tu uweze kuishi kwa muda mrefu zaidi.

Hata hivyo, licha ya kutokuwa na njia za kuzuia saratani ya mapafu, mtu anaweza kujikinga kutokana na saratani hii kwa kutovuta sigara. Kama hujawahi kuvuta sigara wala tumbaku, usianze. Isitoshe, waeleze watoto wako kuhusu madhara ya kuvuta sigara ili waweze kujihami kutokana na ushauri potovu kutoka kwa marafiki wao.

Ikiwa unavuta sigara ama tumbaku wacha. Kuwacha kuvuta hukupunguzia athari za kupata saratani hii ya mapafu. Vile vile, mweleze daktari wako kuhusu uraibu huu ili akuelekeze katika njia ambazo zitakazokusaidia ili kuepuka na kuwacha uraibu huo. Iwapo unaishi na mtu anayevuta sigara, mshauri kuwacha.

Ikiwa hatakusikia, mweleze avutie sigara ama tumbaku yake nje. Hii ni kwa sababu kuwepo na mtu anayevuta kunakuweka katika athari ya kupata kansa hii.

Jizuie kutokana na kemikali zinazosababisha kansa ukiwa kazini. Zingatia masharti uliyopewa na mwajiri wako ili ujikinge. Tano, chagua vyakula vitakavyoujenga mwili wako.

Vyakula vilivyo na vitamini na virutubishi vingi husaidia mwili. Usimeze dawa nyingi za vitamini. Uchunguzi umebainisha kuwa kumeza dawa hizi za vitamini hukuweka katika athari za kupata kansa ya mapafu. Mwisho, kuwa na uzoefu wa kupiga tizi siku nyingi za wiki.