Michezo

Injera tayari kwa raga ya dunia ya IPL World Tens

October 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

COLLINS Injera anatarajia kivumbi cha dunia cha wachezaji 10 kila upande almaarufu ‘The IPL World Tens Series’ kutawaliwa na ushindani mkali na matumizi ya nguvu nyingi kupindukia kuliko jinsi alivyozoea kwenye kipute cha wanaraga saba kila upande.

Kipute cha World Tens kitaanza wikendi hii katika Kisiwa cha Bermuda na kukamilika baada ya majuma matatu. Injera ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya Shujaa, anabashiri mapambano hayo kutamalakiwa pia na hisia kali zitakazochangiwa na msukumamo wa mara kwa mara kati ya wachezaji wakiwania mpira.

“Hali itakuwa tofauti kabisa. Hasira zitapanda, wachezaji wataumizana na uwanja utakuwa mdogo. Hata hivyo, tija na fahari zaidi itakuwa ni fursa ya kucheza na baadhi ya wanaraga wa haiba kubwa zaidi kwenye ulingo wa raga duniani,” akasema Injera ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa trai kambini mwa Shujaa.

Mbali na Injera, wanaraga wengine wa humu nchini ambao watanogesha kivumbi cha World Tens ni Monate Akuei, Willy Ambaka, Oscar Ouma, Oscar Dennis na nahodha wa Shujaa, Andrew Amonde.

Sita hao watakuwa sehemu ya kikosi cha SFX 10 kutoka Cape Town, Afrika Kusini chini ya ukufunzi wa mwanaraga wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Frankie Horne.

“Japo kutakuwa na matukio mengi ya kusukumana, nahisi kwamba hali itakuwa nafuu kuliko jinsi ambavyo ingekuwa iwapo mashindano haya yangehusisha wanaraga 15 kila upande,” akahoji Injera.

Mechi za raundi ya kwanza ya kipute hicho zimeratibiwa kuanza wikendi Oktoba (24-25) kabla ya zile za raundi ya pili kutandazwa kati ya Oktoba 31 na Novemba 1. Fainali za kivumbi hicho kitakachoshirikisha vikosi saba ni Novemba 7 uwanjani National Sports Centre.

Kipute cha World Tens kitafanyika kwa mfumo wa ligi za kawaida ambapo kila kikosi kitacheza na kingine mara mbili kufikia mwisho wa wikendi tatu zijazo.

Mbali na kikosi cha SFX 10 kutoka Cape Town, Afrika Kusini, washiriki wengine ni Asia Pacific Dragons (Singapore), Phoenix (Mashariki ya Kati), London Royals (London), Miami Sun (Florida), Rhinos (California Kusini) na Ohio Aviators (Columbus).

“SFX 10 kinajivunia wanaraga wenye tajriba pevu na uzoefu mkubwa kimataifa. Tumewateua kwa sababu Kenya ni mojawapo ya mataifa ambayo ni ngome ya wanaraga stadi duniani sawa na New Zealand, Fiji, Amerika na Afrika Kusini,” akasema Horne kwa kuthibistisha kwamba SFX 10 kitakuwa chini ya unahodha wa Cecil Afrika kutoka Afrika Kusini.

Kubwa zaidi katika matamanio ya Akuei ni kuona mchezo wa raga ukimsaidia siku moja kusafirisha familia yake kutoka Amerika na kurudi Kenya.

“Hiki kitakuwa kivumbi kikubwa kitakacholeta pamoja wanaraga maarufu na wa haiba ya juu zaidi duniani,” akasema Akuei ambaye ni fowadi wa Kenya Simbas.

“Nalenga sana kusaidia familia yangu na pia kupata hifadhi kambini mwa kikosi kitakachonipa jukwaa zuri zaidi la kujikuza kitaaluma,” akaongeza.

Fowadi huyo anatazamia pia kuwa sehemu ya mechi kadhaa zijazo za Simbas, ikiwemo michuano ya kimataifa ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mnamo 2022.