Makala

RIZIKI: Ukuzaji na uuzaji wa miche wafaidi vijana

October 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER CHANGTOEK

TAKRIBAN kilomita mbili kutoka kwa soko la Manyatta, kwenye barabara ya Manyatta-Kianjokoma, katika Kaunti ya Embu, shamba moja la miche lafahamika kwa wengi.

Hilo ndilo shamba ambalo linamilikiwa na Brian Kimathi na David Kimanthi.

Wawili hao walijitosa katika biashara ya ukuzaji na uuzaji wa miche ya miparachichi na mikadamia. Wanalitumia shamba ekari moja kuiendesha shughuli hiyo.

“Nilijuzwa kuhusu kilimo-biashara hiki na mwenzangu ambaye tunashirikiana naye,” asema Kimathi, ambaye ana umri wa miaka 29.

Mkulima huyo, ambaye anasomea taaluma ya uhasibu katika chuo kijulikanacho kwa jina Achievers College, kilichoko katika Kaunti ya Embu, anasema kuwa walijitosa katika ukulima huo mwaka 2018.

“Sisi huikuza miche ya mikadamia na miparachichi aina ya Hass,” adokeza mkulima huyo, akiongeza kwamba mikadamia imekuzwa kwa shamba nusu ekari, huku miparachichi ikichukua nafasi iliyosalia.

Kimathi anafichua kuwa wakati wa upanzi wa mbegu, wao huzitumia mbolea za kiasili, pamoja na zile za madukani, aina ya DAP, anazosema huboresha ukuaji wa mizizi.

Kabla hawajazipanda mbegu, wao huhakikisha kuwa mbegu ni bora, kwa kuzichambua vyema. Baada ya kuzipanda, hung’oa magugu kitaluni, hunyunyizia maji kwa miche na kuhakikisha kwamba wadudu wanazuiwa, ili wasiiharibu miche. Aidha, huhakikisha kuwa miche yao inaatikwa au kupandikizwa inavyotakikana.

“Kwanza, sisi huanza kwa kuchambua mbegu zilizo bora, kisha tunalowesha kwa maji kwa muda wa saa 24, halafu huanika kwa jua,” asema Kimathi.

“Kisha tunaziweka mbegu kwa kitalu ambapo huchukua muda wa mwezi mmoja ili kuanza kuota,” asema.

Baadaye, wao hupanda kwa karatasi za sandarusi ambapo hukaa kwa muda wa miezi 6 hadi 8, na baadaye huatikwa. Baada ya kuatikwa, miche huchukua muda wa miezi mitatu kabla haijauzwa.

Wahudumu wakihudumu katika shamba la miche eneo la Makutano, Manyatta, Kaunti ya Embu. Picha/ Peter Changtoek

Hata hivyo, kuna changamoto kadha wa kadha, ambazo wawili hao wamewahi kuzipitia. Uhaba wa maji ya kutumia ni mojawapo ya ndaro hizo. Pia, changamoto ya kuisafirisha miche iwafikie wateja wanaoagizia katika maeneo ya mbali, ni changamoto nyingine inayowakabili.

Hali kadhalika, mkulima huyo anasema kuwa kuna baadhi ya magonjwa na wadudu kadhaa, ambao huivamia miche yao.

Mkulima huyo anafichua kuwa wao wana miche ya mikadamia aina tatu; Murang’a 20, Embu 1 na Kiambu.

Wao huiuza miche yao mitandaoni, na kwa wale wanaozuru shambani, kwa bei tofauti tofauti. Kimathi anadokeza kwamba, huuza miche ya mikadamia aina ya Murang’a 20 kwa Sh250 kila mmoja, Embu 1 kwa Sh250 kila mmoja, na miche ya mikadamia aina ya Kiambu kwa Sh250 kila mmoja. Vile vile, huiuza miche ya miparachichi aina ya Hass kwa Sh150, kila mmoja.

“Sisi huiuzia hapa na natumai kuwa kadiri siku zinavyosonga, tutapata wateja kutoka nchi nyingine,” adokeza mkulima huyo, akiongeza kuwa waliutumia mtaji wa Sh200,000 kuanzisha shughuli hiyo.

Mkulima huyo, ambaye ana wafanyikazi sita, anawashauri wale wanaonuia kujitosa katika ukuzaji na uuzaji wa miche kujifunza kutoka kwa wale waliobobea, kwa kuyatembelea mashamba mbalimbali.