Bayern waanza kutetea ufalme wa UEFA kwa kuponda Atletico Madrid 4-0
Na MASHIRIKA
MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) waliendeleza rekodi ya kutoshindwa kwao kwenye soka ya bara Ulaya katika mechi 12 mfululizo baada ya kuanza kampeni za msimu huu kwa kupepeta Atletico Madrid ya Uhispania 4-0 mnamo Oktoba 21, 2020.
Bayern ambao ni miamba wa soka ya Ujerumani, walishuka dimbani kuvaana na Atletico siku 59 tangu wapepete Paris Saint-Germain (PSG) 1-0 jijini Lisbon, Ureno na kutwaa taji la UEFA msimu uliopita chini ya kocha Hansi Flick.
Kingsley Coman aliyefunga bao lililozamisha chombo cha PSG mnamo Agosti 2020, alifunga mabao mawili dhidi ya Atletico kabla ya mengine kufumwa wavuni kupitia Leon Goretzka na Corentin Tolisso.
Ni Real Madrid ya Uhispania na AC Milan ya Italia ndivyo vikosi vya pekee ambavyo vimewahi kuhifadhi ufalme wa taji la UEFA tangu Nottingham Forest wafaulu kufanya hivyo chini ya kocha Brian Clough mnamo 1980.
Hata kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Atletico, Bayern walikuwa wakipigiwa upatu wa kutamba dhidi ya masogora hao wa kocha Diego Simeone.
Coman aliwafungulia waajiri wake karamu ya mabao kunako dakika ya 28 baada ya kushirikiana vilivyo na Joshua Kimmich. Fowadi huyo chipukizi raia wa Ufaransa alichangia mabao mengine yaliyofumwa wavuni na Goretzka na Tolisso kabla ya kucheka tena na nyavu za wageni wao katika dakika ya 72.
Goli hilo la pili la Coman lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na kiungo Thomas Muller. Bayern walifunga jumla ya mabao 43 kwenye kampeni zote za UEFA msimu uliopita wa 2019-20.