Michezo

Wanne waitwa kuwasaidia Lionesses kutamba Botswana

May 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Kevin Wambua amejumuisha wachezaji wanne wapya katika kikosi cha Kenya Lionesses kitakachowania ubingwa katika mashindano ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Afrika ya wanawake jijini Gaborone, Botswana hapo Mei 25-26, 2018.

Wachezaji hao ni Diana Awino, Sarah Oluche, Sophia Ayieta na Prisca Nyerere, ambao Wambua amesema walimridhisha sana mazoezini na pia wakiwakilisha klabu zao mashindanoni jijini Nairobi.

Wanne hawa wanajaza nafasi za Celestine Masinde, ambaye ameshikika kikazi, Rachel Mbogo, ambaye anauguza jeraha, na Stacy Awuor na Doreen Remour, ambao huduma zao hazipatikani wakati huu.

Kenya, ambayo imepoteza dhidi ya Afrika Kusini katika fainali nne mfululizo (mwaka 2014, 2015, 2016 na 2017), ina fursa nzuri ya kutwaa taji baada ya miamba hao kujiondoa. Lionesses imetiwa katika Kundi A linalojumuisha pia Madagascar na Senegal.

Matafa 10 yatawania taji la Afrika. Tunisia, Uganda na Zimbabwe zimekutanishwa katika Kundi B nazo Morocco, Botswana, Mauritius na Zambia zitakabiliana katika Kundi C.

Wambua amefurahishwa na kuingia kwa chipukizi katika kikosi cha watu wazima akisema hana wasiwasi kuhusu baadhi ya wachezaji wanaokaribia kustaafu. Kocha huyu pia alielezea kufurahishwa kwake na Lionesses kushiriki mashindano makubwa matatu katika muda wa miezi miwili pekee.

“Mwaka 2018 umekuwa mzuri sana kwetu. Kushiriki mashindano makubwa matatu katika muda huu mfupi inatutia moyo sana,” Wambua alisema kuhusu ziara ya Lionesses katika shindano la mwaliko la Hong Kong na michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika mwezi Aprili, na Kombe la Afrika litakaloandaliwa Gaborone wikendi hii.

Timu zitakazofika fainali jijini Gaborone zitafuzu kuwania tiketi ya kuingia Raga ya Dunia ya Wanawake ya msimu 2019. Lionesses ilijaribu bahati yake katika mchujo wa kuingia Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019, lakini bila mafanikio.

Licha ya kukosekana kwa Afrika Kusini, ambao ni mahasimu wakuu wa Kenya, Wambua ameonya Kombe la Afrika halitakuwa rahisi. Hata hivyo, Kenya itakuwa na shinikizo kali ya kutwaa taji hasa baada ya kucharaza Afrika Kusini mjini Hong Kong na nchini Australia mwezi Aprili.

Lionesses imeratibiwa kuondoka nchini Mei 24 kuelekea Botswana kwa kindumbwendumbwe hicho.

Kikosi cha Lionesses:

Wachezaji

Philadelphia Olando, Sheila Chajira, Michelle Omondi, Grace Adhiambo, Linet Moraa, Camilla Cynthia, Janet Okello, Judith Auma, Diana Awino, Sarah Oluche, Sophia Ayieta na Prisca Nyerere.

Benchi la kiufundi

Kevin Wambua (Kocha Mkuu), Camilyne Oyuayo (meneja wa timu), Ben Mahinda (daktari wa timu) na Sammy Njogu (kocha wa mazoezi ya viungo).