BBI: Rai ya wabunge dhidi ya upotoshaji
Na CHARLES WASONGA
UONGOZI wa bunge umewaonya Wakenya dhidi ya kutegemea wanasiasa wawasomee na kuwafafanulia kuhusu yaliyomo katika ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) na badala yake waisome na kuielewa kikamilifu.
Wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi katika bunge la kitaifa Amos Kimunya na Kiranja wa Wengi Irungu Kang’ata, wabunge na maseneta 20 kutoka mirengo ya Jubilee na upinzani waliwataka wananchi kujisomea ili wabaini mapendekezo yanayowafaa na yale ambayo wangependa yarekebishwe.
“Baadhi yetu tumeisoma ripoti hiyo na kuridhika kwamba inasheheni masuala yanayotuhusu kama uwakilishi na wajibu wetu kama wabunge. Pia imefafanua kikamilifu masuala yote tisa ambayo yalitajwa kama chanzo cha machafuko ambayo hukumba taifa hili kila baada ya uchaguzi.
“Kwa hivyo, tunataka kuwahimiza Wakenya wote kujisomea ripoti hii wenyewe wala wasiwaruhusu baadhi ya wanasiasa kuwapotosha kwa kudai yote yaliyomo ni mabaya,” Bw Kimunya akasema Alhamisi kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.
Mbunge huyo wa Kipipiri alisema ripoti hiyo ya BBI haipaswi kutumiwa kuwagawanya Wakenya kwa misingi ya “Sisi” dhidi ya “Wao”.
“Ripoti hii inastahili kutuunganisha sote kama taifa,” Bw Kimunya akasema.
Kwa upande wake, Bw Kang’ata alisifia ripoti hiyo iliyopokezwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga mnamo Jumatano katika eneo la Kisii, akisema ina mapendekezo yanayopiga jeki ugatuzi.
“Ripoti hii inaafiki wito wa Seneti kwamba kaunti zinapaswa kuongezwa mgao wa fedha kwani imependekeza kuwa kaunti zitengewe asilimia 35 kutoka asilimia 15 ya sasa. Vile vile, imependekeza kubuniwa kwa hazina ya maendeleo katika wadi, sambamba na malengo ya mswada wangu,” akasema Bw Kang’ata ambaye ni Seneta wa Murang’a.
Saa chache baada ya ripoti hiyo kupokezwa Rais Kenyatta na Bw Odinga, baadhi ya wanasiasa wandani wa Naibu Rais William Ruto walisema wataipinga kwa sababu inapendekeza kubuniwa kwa nyandhifa zao za uongozi.
Wakiongea katika hafla ya mazishi Eldoret, wabunge Oscar Sudi (Kapseret), Didmus Barasa (Kimilili) na Daniel Rono (Keiyo Kusini) walisisitiza watawahimiza Wakenya kukataa ripoti hiyo kwani inawaongezea mizigo.
Wakati huo huo, Jaji Mkuu mstaafu Willy Mutunga amepinga wito wa mageuzi ya Katiba kusudi kuundwe nafasi zaidi za uongozi kama ilivyopendekezwa katika ripoti ya BBI.
Dkt Mutunga alisema suluhu kwa matatizo yanayozonga taifa hili si kuanzishwa kwa nyadhifa za Waziri Mkuu na manaibu wake wawili akisema tatizo kubwa ni “utovu wa nidhamu miongoni mwa viongozi wetu”.
“Nashindwa kukubali kwamba Katiba inafaa kufanyiwa mabadiliko kwa sababu hiyo; ikiwa ni kweli kwamba ripoti ya BBI inapendekeza kuwe na nyadhifa za Waziri Mkuu na manaibu wake. Chimbuko la matatizo yanayolizonga taifa hili sio ukosefu wa nyadhifa kama hizo bali ni uhaba wa viongozi waadilifu,” akasema Jumatano usiku kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen.
Dkt Mutunga aliongeza kile kinahitajika nchini ni utekelezaji kikamilifu wa Katiba ya sasa ambayo alisema ina vipengele vinavyohimiza uongozi bora.