• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Obiri kustaafu rasmi mbio za uwanjani na kuhamia barabarani baada ya Olimpiki za Tokyo

Obiri kustaafu rasmi mbio za uwanjani na kuhamia barabarani baada ya Olimpiki za Tokyo

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA mara mbili wa dunia katika mbio za mita 5,000 Hellen Obiri hatatetea taji lake kwenye mbio za nyika za dunia mnamo 2021 jijini Bathurst, Australia.

Badala yake, mwanariadha huyo atakuwa akilenga kuvuma katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo nchini Japan kabla ya kustaafu rasmi kwenye mbio za uwanja.

Kwa mujibu wa Obiri, kubwa zaidi katika malengo yake ni kustaafu kwenye ulingo wa riadha akijivunia nishani ya dhahabu ya Olimpiki katika mbio za mita 5,000.

“Nishani ya Olimpiki ndiyo inayoongoza orodha ya medali nitakazotaka kutwaa msimu ujao ambao natazamia kwamba utakuwa na kalenda yenye mrundiko wa mashindano mbalimbali. Nafanya niwezalo kuhakikisha maazimio yangu hayatikiswi na mapambano mengine kabla ya kutwaa dhahabu ya Olimpiki,” akasema Obiri ambaye atanogesha mbio mbio za mita 1,500 jijini Tokyo.

Obiri amefichua kwamba tayari ameanza kushiriki mazoezi mepesi kwa minajili ya kujiandaa kwa mbio za msimu ujao katika Diamond League atakazoshiriki kujinolea kwa michezo ya Olimpiki mnamo Julai 2021.

“Ratiba yangu kwa minajili ya msimu ujao wa 2021 imejipanga yenyewe na sioni uwezekano wa kunogesha mbio za nyika za dunia,” akaongeza Obiri.

Baada ya kushiriki mashindano ya Olimpiki, Obiri ambaye pia ni bingwa Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 5,000, amefichua mipango ya kujitosa katika ulingo wa mbio za masafa marefu barabarani.

“Michezo ya Olimpiki itakuwa yangu ya mwisho kushiriki uwanjani kwa sababu napania kujitosa kwenye ulingo wa mbio za barabarani. Hatua yangu hiyo itawapa chipukizi wanaoinukia katika mbio za masafa ya kadri kudhihirisha ukubwa wa uwezo wao uwanjani,” akaeleza.

Obiri alijizolea nishani ya fedha kwenye mbio za mita 5,000 kwenye Olimpiki zilizopita za 2016 jijini Rio, Brazil baada ya kuzidiwa maarifa na Vivian Cheruiyot. Medali ya dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki ndiyo ya pekee anayoikosa kwenye kapu lake la nishani.

Akiwa miongoni mwa wanariadha wa kike wanaojivunia mafanikio makubwa zaidi katika ulingo wa riadha humu nchini, Obiri anajivunia pia kutwaa ubingwa wa Afrika katika mbio za mita 1,500 jijini Marrakesh, Morocco mnamo 2015 kabla ya kuibuka bingwa wa Afrika katika mbio za mita 5,000 mjini Asaba, Nigeria mnamo 2018.

Alijizolea nishani ya dhahabu kwenye mbio za dunia za mita 3,000 jijini Istanbul, Uturuki mnamo 2012 kabla ya kuongoza Kenya kuvunja rekodi ya dunia kwenye mbio za dunia za kupokezana vijiti vya 4×1,500m mnamo 2014 jijini Nassau, Bahamas. Obiri alitawazwa malkia wa mbio za nyika dunia mnamo Machi 2019 jijini Aarhus, Denmark.

You can share this post!

KAMAU: Wakati ni sasa hivi kwa Rais kujiandikia historia

Ni tabia mbaya kuanzisha vyama vya akiba na mikopo kwa...