• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 2:37 PM
Son sasa kuwa miongoni mwa wanasoka wanaodumishwa kwa ujira mnono zaidi Spurs

Son sasa kuwa miongoni mwa wanasoka wanaodumishwa kwa ujira mnono zaidi Spurs

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Son Heung-min anatarajiwa sasa kutia saini mkataba mpya wa miaka mitano utakaomfanya miongoni mwa wanasoka wanaodumishwa kwa mshahara wa juu zaidi kambini mwa Tottenham Hotspur.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, Spurs wanatarajiwa kuongeza ujira wa Son hadi kufikia Sh28 milioni kwa wiki. Makubaliano hayo yatarasimishwa wiki ijayo.

Tottenham ni kati ya vikosi vilivyojishughulisha zaidi katika soko la uhamisho wa wachezaji muhula huu baada ya kujinasia huduma za wanasoka saba wapya, akiwemo Joe Rodon aliyeagana na Swansea City kutoka Ligi ya Daraja la Chini (Championship).

Son, 28, amekuwa tegemeo kubwa kambini mwa Spurs baada ya kuwafungia mabao manane kutokana na mechi saba zilizopita katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kuwepo kwa Gareth Bale, Harry Kane na Son, kunatarajiwa sasa kufanya Spurs kuwa miongoni mwa klabu zinazojivunia wavamizi mahiri zaidi katika soka ya bara Ulaya.

Bale alisajiliwa na Tottenham kutoka Real Madrid kwa mkopo na atakuwa akidumishwa kwa mshahara wa Sh30 milioni kwa wiki kambini mwa waajiri wake hao wa zamani.

Malipo ambayo Son kwa sasa atakuwa akipokea kambini mwa Tottenham yanamweka katika orodha ya masogora wanaodumishwa kwa gharama ya juu zaidi katika kikosi hicho, wakiemo Kane, Bale, Tanguy Ndombele, Serge Aurier, Dele Alli, Lucas Moura na kipa Hugo Lloris.

Son anaingia katika miaka miwili ya mwisho ya mkataba wake na Tottenham mwishoni mwa msimu huu. Hofu zaidi ya Tottenham ni uwezekano wa kupoteza maarifa ya fowadi huyo jinsi ilivyowatokea Christian Eriksen.

Kiungo huyo raia wa Denmark aliyoyomea Inter Milan kwa Sh2.3 bilioni pekee mapema mwaka 2020 akisalia na miezi 12 kwenye kandarasi yake na Spurs.

Kwa mujibu wa Levy, fedha ambazo Spurs walivuna kutokana na mauzo ya Eriksen ilikuwa robo ya thamani yake sokoni wakati huo.

Mbali na Son, wanasoka wengine wanaotarajiwa kurefusha mikataba yao kambini mwa Tottenham hivi karibuni ni Serge Aurier na Erik Lamela.

You can share this post!

City Stars wafichua malengo yao baada ya kumtwaa beki...

RIZIKI: Atumia elimu, ujuzi wake wa ukulima kuwaelimisha...