• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 AM
MPIRA WA VIKAPU: Okari Ongwae afungia Bakken Bears alama 18 akiisaidia kupiga Team FOG Naestved 110-80

MPIRA WA VIKAPU: Okari Ongwae afungia Bakken Bears alama 18 akiisaidia kupiga Team FOG Naestved 110-80

Na GEOFFREY ANENE

TYLOR Okari Ongwae amefungia Bakken Bears alama 18 mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Mpira wa Vikapu ya Wanaume ya Denmark wakikung’uta wageni Team FOG Naestved 110-80 mjini Aarhus, Jumamosi.

Nyota huyo Mkenya aliyeibuka mfungaji bora kwenye mashindano ya Bara Afrika (AfroCan) mjini Bamako nchini Mali mwaka 2019, alichangia alama 13 katika kipindi cha kwanza ambacho Bears iliongoza 56-34.

Ongwae, 29, ambaye yuko katika timu ya Kenya itakayopigania tiketi ya kuingia Kombe la Afrika (AfroBasket) mjini Kigali nchini Rwanda mwezi ujao, alifunga alama moja chache kuliko Mwamerika Deshawn Stephens aliyeibuka mfungaji bora katika mchuano huo wa Ligi Kuu.

Mwamerika Glenn Cosey na raia wa Senegal Michel Diouf ni wachezaji wengine wa Bears waliofunga juu ya alama 10 naye Anto Gadja Harbo akafungia Naestved alama nyingi (15).

Bears inaongoza Kundi A kwenye ligi hiyo kwa alama nane baada ya pia ya kushinda Stevnsgade (105-55), Vaelose (106-74), Amager (128-59) na kupoteza dhidi ya Randers 91-82.

Vijana hao wa kocha Steffen Wich waliingia mchuano dhidi ya Naestved wakiuguza kichapo cha alama 98-73 kutoka kwa Iberostar Tenerife kwenye Klabu Bingwa Ulaya kwenye Kundi A nchini Uhispania hapo Oktoba 20.

Kwenye Klabu Bingwa, Bears pia wamekutanishwa na Dinamo Sassari (Italia) na Galatasaray Doga Sigorta (Uturuki).

Aidha, timu ya Kenya almaarufu Morans tayari imeanza mazoezi jijini Nairobi kujiandaa kuvaana na Senegal, Angola na Msumbiji katika mechi za Kundi B za kuingia AfroBasket zitakazofanyika kati ya Novemba 27,2020 na Februari 21, 2021. Timu tatu za kwanza zitajikatia tiketi ya kuwa nchini Rwanda kwa dimba hilo la mataifa 16.

  • Tags

You can share this post!

Montreal Impact yapoteza mchezo dhidi ya Philadelphia Union

El CLASICO: Real Madrid yaizidi maarifa Barcelona