• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Hofu Barcelona baada ya tegemeo Coutinho kupata jeraha la paja

Hofu Barcelona baada ya tegemeo Coutinho kupata jeraha la paja

Na MASHIRIKA

KIUNGO Philippe Coutinho wa Barcelona atakosa mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) itakayowakutanisha waajiri wake na Juventus mnamo Oktoba 28 jijini Turin, Italia.

Hii ni baada ya nyota huyo wa zamani wa Liverpool kupata jeraha la paja wakati akichezea Barcelona kwenye gozi la El Clasico lililowashuhudia wakipokezwa kichapo cha 3-1 uwanjani Camp Nou mnamo Jumamosi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Barcelona, urefu wa muda ambao Coutinho atahitaji nje ya uwanja utategemea tathmini itakayotolewa na madaktari Jumatatu.

Licha ya kupata jeraha mwanzoni kwa kipindi cha pili, Coutinho alichezewa kwa dakika zote 90 katika mchuano kati ya Barcelona na Real. Nyota huyo alichezea Bayern Munich ya Ujerumani kwa mkopo wa mwaka mmoja katika msimu mzima wa 2019-20 na akawaongoza kutia kapuni mataji matatu – German Cup, Bundesliga na UEFA.

Coutinho ambaye amechezeshwa na Barcelona mara tano msimu huu, alisajiliwa na Barcelona kutoka Liverpool kwa kima cha Sh14 bilioni mnamo Janauri 2018.

Hata hivyo, Coutinho alitatizika sana kufufua makali aliyokuwa akijivunia uwanjani Anfield baada ya kuingia katika sajili rasmi ya Barcelona.

Kushindwa kwake kutamba ugani Camp Nou ni kiini cha Barcelona kumtuma kwa mkopo hadi Bayern. Japo ilitarajiwa kwamba Bayern wangalikuwa wepesi wa kumpokeza mkataba wa kudumu, mabingwa hao wa Bundesliga hawakuonyesha ari ya kuziwania huduma za nyota huyo mzawa wa Brazil.

Badala yake, alianza kuhusishwa na uwezekano mkubwa wa kuingia kambini mwa Leicester City, Everton, Chelsea na Man-United kabla ya kurejea Barcelona.

You can share this post!

Montreal Impact yapata pigo katika juhudi zake MLS

Wanabondia Fury na Joshua kunogesha mapigano yao jijini...