• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
MOKUA: Urafiki wa kweli ni njia hakika ya kuimarisha afya ya akili

MOKUA: Urafiki wa kweli ni njia hakika ya kuimarisha afya ya akili

NA HENRY MOKUA

Kila uchao tunakabiliana na hitaji la mtu wa kusema naye kututua mzigo wa kimhemko tunaobebeshwa na changamoto za siku hadi siku. Machungu yanapozidi kuwa pumzi ya uhai wetu kwa kutusonga bila kikomo, inatulazimu kutafuta msaada unaofikilika.

Ijapo tunamtegemea Mwenyezi Mungu kutufaa katika nyakati kama hizo, twahitaji pia watu walio karibu nasi wanaoweza kutuangazia kama miale ya jua na kuziyeyusha huzuni za mioyoni mwetu.

Nimewaona wanafunzi kadha waliojitenga kwa kuhisi kwamba kuwa na rafiki ni kujiruhusu kuvurugiwa njozi zao lakini wakaishia kuwa na upweke unaowadhuru pakubwa kisaikolojia, kimhemko na kijamii. Ingawa wengi wao huutetea huu mtindo wa maisha, haufai.

Kila mmoja wetu ahitaji mtu wa kumsikiliza! Unapolisherehekea tukio la fanaka, sherehe yenyewe inafana zaidi ambapo unajumuika na mwenzio unayemthamini. Unapoipitia hali ngumu, unapata nafuu hata zaidi kusikilizwa na mtu umthaminiye na akuthaminiye pia.

Kwa msingi huu, wazia kuwa na rafiki wa kusema naye na kushiriki naye furaha na karaha yako. Ukishampata, fanya mazoea kujieleza kwake inapobidi kuhusu hisia za ndani za moyoni mwako. Hii ni njia iliyothibitika ya kujipunguzia msongo na kuyafurahia maisha licha ya matatizo yanayokukabili.

Jambo jingine analoweza kukufaa kwalo rafiki yako wa karibu ni kukunasihi kuhusu changamoto za siku baada ya siku. Ilhali kusikiliza kuna manufaa makubwa, inapowezekana aliyekusikiliza akakunasihi pia, unakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufanya uamuzi kuhusu hatua mwafaka ya kuchukua. Wakati mwingine unagundua kwamba tatizo lako si zito unavyoliona kutokana na nasaha unayoipata na mibadala ya kulitatua.

Rafiki ni wenzo wa kuhimizana. Ili kuzifikilia njozi mbalimbali tulizo nazo, kuna hitaji kubwa la kuwa na mtu mwenye mtazamo chanya wa kuhimizana naye. Unapokuwa na rafiki awezaye kukuhimiza na kukuhamasisha kwamba ndoto zako zinafikilika, unakuwa na hazina ya pekee usiyopaswa kuichukulia hivi hivi.

Wapaswa kuwa katika mstari wa mbele katika kumhimiza mwenzio ili umchochee kukuhimiza hali kadhalika. Mkilifanya jambo hili mazoea yenu mna hakika ya kufaana pakubwa na kupiga hatua ambazo msingezipiga bila ukuruba huo wa karibu.

Waonaje ukiwa kimbilio la mwenzio anapokabiliwa na hali ngumu? Kutokana na hitaji kubwa la marafiki wa kweli, haihalisi kuwazia kumpata rafiki kama huyo iwapo wewe mwenyewe hutojituma kuwa rafiki wa awali. Kudumu kuyafanya kwa wenzio niliyokwisha kuyataja – yaani kuwasikiliza wenzio, kuwanasihi na kuwahimiza ni namna ya kuuimarisha uchangamfu wako, afya yako ya kiakili, kimhemko, kisaikolojia na kijamii.

Ili kuifanikisha azma hii ya kuwa rafiki wa kutegemewa, jifunze kuwa mkweli. Kuwa mkweli kuna namna fulani ya kuwavutia watu na kutambuliwa. Huenda usifanikiwe mia fil mia katika hili lakini ukiamua na kuazimia toka moyoni mwako waweza kuwa mkweli ikiwa hujawa. Mtajie mwenzio kosa lake linapokubainikia; hii ndiyo njia hakika ya kumkuza. Jizoeze pia kumpongeza kila anapostahiki. Kuyafanya haya huchangia mno kukuza urafiki wa kweli na wa kutegemewa.

Jambo jingine la msingi la kukufanya uwe rafiki mwema ni kuwa msiri. Mwenzio anapokuambia siri za maisha yake, jifunze kuziweka siri zenyewe.

Unapofanya vile, unaibuka kuwa mtegemewa mkubwa kwa mwenzio. Kisa na sababu, ni watu wachache wawezao kuweka siri na unatarajia kwamba mengi ya machungu waliyo nayo watu ni siri. Hebu wazia kuwa mmoja katika hao wachache na utakuwa baraka ya pekee kwa wanaokuzunguka.

Hatimaye, jifunze kuwa na mtazamo mpana. Watu wengi huwaumiza wenzio waliowategemea kuyaponya majeraha yao kwa kuwakwaruza pale pale walipoumia. Ni jambo la busara kumsikiliza mwenzio kwa makini kisha ukatoa wazo lako kwa tahadhari huku ukitia maanani hisia zake. Hata ambapo kukosolewa kwahitajika, fanya vile kwa tahadhari usije ukazua hatari.

Mungu ana namna ya kulipa juhudi hizi za kuwaumbia wengine furaha badala ya kuwa mtumiaji daima wa furaha iliyoumbwa na wengine. Hebu pokea hizo baraka kwa kuwa rafiki wa kweli na wa kutegemewa.

You can share this post!

AFYA: Miaka 17 baadaye bado chozi linamtiririka…

Afisi ya Fedha Mandera yafungwa