• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Umuhimu wa kuwa na ukomavu kukabili mahangaiko ya dunia

Umuhimu wa kuwa na ukomavu kukabili mahangaiko ya dunia

Na SAMMY WAWERU

Aghalabu unapopitia mazito maishani, kipindi cha muda huo huwa cha hali ngumu ukitafakari namna ya kujinusuru.

Kwa waliopoteza wapendwa wao, huwa ni hali ya kilio na majonzi, mwathiriwa akihitaji mtu wa kuwa karibu naye na kumfariji.

Lakini licha ya hayo, maisha sharti yasonge mbele, liwe liwalo. Hata hivyo, kidonda cha moyo huchukua muda kupona, na kinapopona makovu ya ‘majeraha’ husalia.

Ni mjadala uliobuliwa katika kongamano la wanaume waliopewa talaka na wake wao au waliofiwa na kuachiwa majukumu kulea watoto, yaani ‘singo fatha’.

Katika semina hiyo iliyoandaliwa katika Kanisa la Kingdom Seekers – Thika Road, majuzi, Askofu Frank Moses kutoka Nigeria alilichanganua kwa mapana na marefu.

Kwa usaidizi wa maandiko ya Biblia, Askofu huyo alitumia mfano wa watoto wa kiume waliouawa Yesu alipozaliwa.

“Kuna vita visivyoisha kwa mtoto wa kiume. Vita vinapozuka katika taifa, wanaume ndio huumia zaidi. Yesu alipozaliwa, unajua ni watoto wangapi wa kiume waliuawa na Mfalme Herode?

“Kimsingi, wanaume hupitia mengi na wanahitaji ukomavu wa kiroho kupiku majaribu yanayowazingira.” Askofu Frank akafafanua, pia akitumia mfano wa Mfalme Samueli.

“Mungu alimuuliza Mfalme Samueli ataendelea kuhuzunika hadi lini baada ya kumkataa Saulo kuwa Mfalme…Alimfunza mengi na alimtaka awe imara…” akaelezea.

Aidha, kwa kutumia mukhtadha huo, Askofu Frank alisema tunapaswa kufanya nyoyo zetu kuwa nyepesi na kuzifunza kusahau magumu tunayopitia na pia kusamehe waliotukosea kwa njia moja ama nyingine, akisema hiyo ni mojawapo ya njia kurithi Ufalme wa Mwenyezi Mungu.

“Ikiwa huna moyo wa kusamehe, usiingie katika ndoa kwa sababu ni ‘taasisi’ ya moyo. Kama mume, lazima uwe na uwezo kusuluhisha matatizo katika ndoa na kuisimamisha iwe ya kutamanika,” Mchungaji huyo akahimiza singo fatha waliojitokeza kuhudhuria kongamano hilo ambalo pia lilikuwa na wanawake kadhaa.

Semina hiyo iliandaliwa na Mwinjilisti Peris Wakarura, ambaye ni singo matha wa watoto sita. Mtumishi huyo wa Mungu amekuwa katika mstari wa mbele kusaidia wasiojiweza katika jamii, wakiwemo mayatima na wajane.

Alichukua hatua hiyo baada ya kuhusika katika ajali mbaya na punda, wakati akisafirisha mizigo mwaka wa 2007. Ni ajali iliyoathiri uti wake wa mgongo na kumlazimu kutumia kiti cha magurudumu, kinachotumiwa na watu wenye matatizo ya kutembea.

Kulingana na Peris, ambaye ni Mchungaji Mmishonari aliendelea katika hali hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu, mfululizo.

Ni majeraha mabaya yaliyomuacha akiwa singo matha, mumewe alipomtoroka baada ya kuona ameshindwa kutembea. “Watu walinisema kwa mafumbo, ila Mungu aliniponya. Nilishawasamehe wote walionisengenya na kunikosea,” Peris anadokeza.

Kulingana na Askofu Frank Moses, hatua ya msamaha aliochukua Peris inaonyesha ukomavu wa kiroho, unaopaswa kuigwa, akisema ni moyo na matendo yanayomridhisha Mungu.

Askofu huyo pia anasema ndoa yake ilipokuwa changa, ilikuwa yenye changamoto chungu nzima, kwa kile alitaja kama kutarajia makuu kutoka kwa mkewe.

“Kwa sababu ya kunyimwa haki ya ndoa, nilienda nje. Nje ya ndoa, nilikutana na shetani naye akanibusu. Hata hivyo, mimi sasa ni kiumbe mpya nilimsamehe mke wangu kwa kunishurutisha nizini, nilimpa uhuru wa kujitawala na huo ukawa mwanzo wa furaha katika maisha yangu,” Mchungaji akasema, akihimiza haja ya uaminifu na kusamehe katika ndoa.

Askofu huyo anasema msingi na chanzo cha masaibu ya ndoa ni kudhania mpenzio ni malaika atakayekutimizia kila kitu, ilhali sivyo.

Muhimu zaidi, Frank anasema ni kushirikisha Mwenyezi Mungu kwa njia ya maombi.

Kilele cha mafunzo ya Askofu huyo kikawa singo fatha kadhaa kueleza bayana yaliyo moyoni, baadhi yao wakihoji wangali mateka wa minyororo ya mazito waliyopitia kwenye ndoa na ambayo mara kwa mara hufufua makovu ya majonzi.

“Iwapo haupo tayari kubadilika kama mwanamume na kuwa mtiifu, hata makongamano ya aina hii yatakuwa ya kazi bure. Hayatakusaidia! Kina baba na mama sisitizieni utiifu na uaminifu kwenye ndoa. Waume muyatekeleze majukumu yenu kama vichwa vya familia, nanyi wake muwe wanyenyekevu. Msijisumbue na wanandoa wasio watiifu,” Askofu Frank akashauri.

Kwa wale ambao wangali mateka wa msongo wa mawazo, anasema ni muhimu wajinasue kwa kujieleza wapate usaidizi wa ushauri nasaha, ili wafungue chapta au ukurasa mwingine wa maisha.

Kongamano hilo pia lilihudhuriwa na mapasta kadhaa, baadhi yao wakiwa singo fatha baada ya kufiwa na wake.

You can share this post!

Mzee Makanyaga azikwa katika makaburi ya Kariorkor

Afunguka jinsi maisha yalimtesa, mama yake akiolewa na...