• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
Olunga, Wanyama wapongeza Mandela kujiunga na Mamelodi Sundowns

Olunga, Wanyama wapongeza Mandela kujiunga na Mamelodi Sundowns

Na GEOFFREY ANENE

MSHAMBULIAJI Michael Olunga na kiungo Victor Wanyama wamepongeza Brian Mandela Onyango katika safari yake mpya baada ya beki huyo kuajiriwa na miamba wa Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns mnamo Oktoba 29, 2020.

Mandela, 26, ambaye hakuwa na klabu tangu apigwe teke Julai 1 mwaka 2019 na Maritzburg United inayoshiriki Ligi Kuu, amejiunga na Sundowns kwa kandarasi ya miaka mitatu.

Mnamo Oktoba 15, washiriki wapya wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini Tshakhuma Tsha Madzivhandila (TTM) walikuwa wamedai kusajili Mandela. Hata hivyo, alipuuzilia mbali habari hizo.

Hapo Oktoba 29, beki huyo anayechezea timu ya taifa ya Kenya alithibitishwa kuwa mali ya Sundowns ilipochapisha picha yake na ikisema imekamilisha kumsaini.

Kupitia mtandao wake wa Twitter, Wanyama, ambaye ni mchezaji wa Montreal Impact inayoshiriki Ligi Kuu ya Amerika na Canada (MLS), alisema, “Hongera ndugu yangu Brian Mandela. Wakati wa kung’ara ni sasa.”

Olunga, ambaye anaongoza ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu nchini Japan akichezea Kashiwa Reysol, hakuachwa nyuma katika kupongeza Mandela.

“Nisaidieni kumpongeza Brian Mandela kwa kujiunga na Mamelodi Sundowns. Endelea kung’aa,” aliandika Olunga kwenye mitandao wake wa Facebook.

Rais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) Nick Mwendwa amepongeza Mandela kwa kujiunga na Sundowns akisema, “Hongera Mandela…Komoro imechelewa!!!”

Mandela alichezea Posta Rangers na Tusker nchini Kenya kabla ya kujiunga na Santos nchini Afrika Kusini mnamo Agosti 12 mwaka 2012 na kisha Maritzburg mnamo Agosti 3 mwaka 2015. Alipata umaarufu mkubwa akiwa Maritzburg aliyoichezea jumla ya mechi 86 na kuifungia mabao manane.

Jeraha baya la goti lilimweka mkekani wakati Kombe la Afrika (AFCON) 2019 nchini Misri. Alionyesha amepona kabisa jeraha hilo na yuko fiti pale alipocheza dakika 86 timu ya Kenya ikilemea Chipolopolo ya Zambia 2-1 katika mechi ya kujipima nguvu jijini Nairobi mnamo Oktoba 9.

Mandela pia yuko katika kikosi cha Harambee Stars kitakachopepetana na wanavisiwa wa Komoro katika mechi za Kundi G za kufuzu kushiriki AFCON2021 zitakazosakatwa Novemba 11 jijini Nairobi na Novemba nchini Komoro.

  • Tags

You can share this post!

Wanyama kuwania tuzo ya Mchezaji Mpya Amerika na Canada

JS Kabylie yatangaza kikosi chake cha msimu mpya akiwemo...