• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 11:55 AM
JS Kabylie yatangaza kikosi chake cha msimu mpya akiwemo Masud Juma

JS Kabylie yatangaza kikosi chake cha msimu mpya akiwemo Masud Juma

Na GEOFFREY ANENE

MVAMIZI wa timu ya taifa ya Kenya, Masud Juma amejumuishwa katika kikosi cha timu ya JS Kabylie kitakachoshindania mataji nchini Algeria kwenye msimu 2020-2021.

Juma,24, ambaye klabu hiyo yake ilitangaza mwezi Septemba aliugua na kupona virusi vya corona, ametajwa katika orodha ya washambuliaji tisa.

Si kawaida kwa mchezaji kutajwa katika kikosi cha msimu jinsi alivyofahamu Mjerumani Mesut Ozil baada ya kocha Mhispania Mikel Arteta kumuacha nje ya vikosi vitakavyowakilisha klabu ya Arsenal kwenye Ligi Kuu ya Uingereza na Ligi ya Bara Uropa.

Juma alijiunga na Kabylie mnamo Julai 25 mwaka 2019 kutoka Al-Nasr Benghazi nchini Libya kwa kandarasi iliyoratibiwa kukamilika Juni 30 mwaka 2020, lakini ikaongezwa.

Majuzi, mashabiki wa Kabylie walitaka Juma aondolewe kikosini kwa kuwa aliichezea mechi chache sana, huku muda mwingi akiuguza majeraha. Hata hivyo, amepona na mashabiki wa klabu hiyo wanasema wako tayari kuona atakachowafanyia uwanjani msimu huu.

Juma alisakatia Kabylie michuano 10 ligini na mbili kwenye Klabu Bingwa Afrika msimu uliopita. Hakupachika bao, ingawa alichangia pasi moja iliyozalisha goli ligini.

Ametajwa katika kikosi cha Kenya kitakachovaana na wanavisiwa wa Komoro mnamo Novemba 11 na Novemba 15 kwenye mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2021. Juma alishiriki mechi ya kirafiki ya Harambee Stars ilipokung’uta Chipolopolo ya Zambia 2-1 jijini Nairobi mwezi uliopita (Oktoba 9).

 

Orodha ya wachezaji wa JS Kabylie wa msimu 2020-2021:

Makipa – Benbot, Becheker;

Mabeki – Ait Abdessalem, Mebarki, Bencherifa, Tizi Bouali, Souyed, Haddouche, Chikhi;

Viungo – Raiah, Oukaci, El Orfi, Aguieb, Derragi, Benchaira, Benabdi, Bounoua, Daibeche; Washambuliaji – Hamroune, Bensayah, Al Tubal, Masud Juma, Boulahya, Kadour Cherif, Nezla, Fellahi, Loucif.

  • Tags

You can share this post!

Olunga, Wanyama wapongeza Mandela kujiunga na Mamelodi...

Sh50 bilioni zaishia msituni