• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Nyota wa Ingwe ahamia Nzoia Sugar kwa mkopo

Nyota wa Ingwe ahamia Nzoia Sugar kwa mkopo

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO mpya wa Nzoia Sugar, Dan Musamali, amesema kujiunga kwake na wanasukari hao kutoka AFC Leopards kutampa jukwaa maridhawa la kujikuza zaidi kitaaluma.

Mwanafunzi huyo wa zamani wa Shule ya Upili ya St Anthony’s Kitale, ameahidi kufanya makuu kambini mwa Nzoia na kurejea Ingwe kwa matao ya juu zaidi mwishoni mwa kipindi chake cha mkopo.

“Hii ni nafasi yangu ya kupata muda zaidi wa kusakata soka uwanjani na kujiimarisha kitaaluma. Leopards kwa sasa wanajivunia idadi kubwa ya wanasoka stadi na lengo langu ni kurejea kambini mwao na kupata nafasi katika kikosi cha kwanza,” akasema Musamali.

Kwa mujibu wa mkataba aliopokezwa na Leopards, kiungo huyo atakuwa huru kuchezea Nzoia dhidi ya Ingwe katika mashindano yote ya msimu ujao.

Musamali aliingia katika sajili rasmi ya Leopards mnamo Septemba 2019 baada ya kuagana na St Anthony’s. Alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa wa kitaifa wa Michezo ya Shule za Upili jijini Kisumu mnamo 2019 baada ya kuongoza St Anthony’s Kitale kuwapepeta Dagoretti High 5-4 kupitia mikwaju ya penalti.

Kwa kuingia katika sajili rasmi ya Nzoia, Musamali anaungana na nahodha wa zamani wa St Anthony’s Kitale, Tyson Kapchanga.

Mwenyekiti wa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Soka ya Kenya, Evance Kadenge, pia amethibitisha kwamba wachezaji tisa wameagana rasmi na kikosi hicho hadi kufikia sasa muhula huu.

“Tumekatiza uhusiano na wachezaji ambao benchi ya kiufundi ilihisi kwamba hawakuridhisha wala kufikia kiwango cha matarajio ya usimamizi kufikia mwisho wa msimu wa 2019-20,” akasema Kadenge.

Kwa mujibu wa Kadenge, Nzoia Sugar bado wana azma ya kuvunja ndoa na wanasoka kadhaa kabla ya muhula huu wa uhamisho wa wachezaji kufungwa rasmi.

“Lengo letu ni kusalia na idadi ya wachezaji ambao tunaweza kumudu mahitaji yao kifedha. Iwapo kuna yeyote atakayetaka kuagana nasi, basi yuko radhi kufanya hivyo. Hatutamzuia mchezaji yeyote kuondoka kwa lengo la kutafuta hifadhi mpya, ambayo kulingana naye, itampigisha hatua kubwa zaidi kitaaluma,” akaongeza Kadenge.

Miongoni mwa sajili wapya wa Nzoia Sugar kufikia sasa ni kipa Mustapha Oduor, Moses Mudavadi na Cliff Kasuti — wote kutoka Bandari FC.

Wengine ni mvamizi Felix Oluoch (Posta Rangers), kiungo Eric Mango (KCB) na Kapchanga. Beki Kevin Maliachi alijiunga na wanasukari hao baada ya kuagana na APS Bomet inayoshiriki Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL). Hadi walipoingia katika sajili rasmi ya Nzoia Sugar, Brian Wanyonyi na Jeremiah Juma hawakuwa na klabu.

Mohammed Nigol, Robert Abonga, Chris Wesamba, Masoud Juma, Abraham Kipkosgei, Faraj Kibali, Boris Kwezi, Jeremiah Wanjala na Vincent Odongo aliyeyoyomea Kariobangi Sharks ni miongoni mwa wachezaji ambao wamekatiza uhusiano na Nzoia Sugar ambao kwa sasa wanatafuta kocha mpya.

“Tumeanza mchakato wa kumwajiri mkufunzi mpya ambaye ana leseni ya daraja la C kutoka kwa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF). Hayo ndiyo masharti kwa kocha yeyote anayedhibiti mikoba ya kikosi cha Ligi Kuu ya Kenya,” akasema Kadenge kwa kufichua kwamba tayari wamepokea maombi ya kazi kutoka kwa wakufunzi 10.

“Idara yetu inayoshughulikia masuala ya ajira inatazamiwa kuandaa orodha fupi ya wote waliotuma maombi ya kazi kabla ya kutangaza siku ya kuanza kwa mahojiano. Tunaazimia kupata kocha mpya chini ya kipindi cha wiki mbili zijazo,” akasisitiza Kadenge.

Kadenge alipokezwa uenyekiti wa Nzoia mnamo Februari 2020 baada ya kuondoka kwa Yappets Mokua. Nzoia Sugar hawajawahi kuajiri kocha tangu Mei 2020 baada ya kuondoka kwa Collins ‘Korea’ Omondi. Mikoba iliyoachwa na Korea imekuwa ikishikiliwa kwa muda na Sylvester Mulukurwa ambaye ni miongoni mwa waliotuma maombi ya kazi ya ukufunzi kambini mwa wanasukari hao.

Musamali alitumwa na Leopards kwa mkopo kambini mwa Nzoia baada ya mabingwa hao mara 13 wa KPL kujinasia huduma za wanasoka wazoefu zaidi msimu huu.

Kati ya wachezaji hao ni kiungo mkabaji raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo), Fabrice Mugheni aliyetokea Rayon Sports nchini Rwanda, Bienvenue Shaka wa Burundi aliyeagana na Etoile Sportif du Sahel ya Tunisia, kipa John Oyemba na fowadi Harrison Mwendwa kutoka Kariobangi Sharks.

Chini ya kocha Anthony Kimani, Leopards kwa sasa wanajifua mjini Iten kwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa 2020-21.

  • Tags

You can share this post!

Jumwa na mlinzi wake ni wapenzi – Korti

Kenya kuwa mwenyeji wa marudiano ya mechi ya AFCON kati ya...