Kipchoge na mwanavoliboli Janet Wanja washinda tuzo
Na GEOFFREY ANENE
MWANARIADHA Eliud Kipchoge na mwanavoliboli Janet Wanja wameshinda vitengo vya wanamichezo maridadi kwenye tuzo za Couture Africa Style jijini Nairobi mnamo Jumamosi.
Katika tuzo hizo zilizofanyika katika hoteli ya Emara Ole Sereni, mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 ya wanaume Kipchoge aliwalemea wanariadha George Manangoi na David Rudisha, wanasoka McDonald Mariga na Ronald Okoth na mchezaji wa raga Billy Odhiambo katika kitengo cha wanaume.
Bingwa huyo wa Olimpiki, ambaye majuzi alimaliza mbio za London Marathon katika nafasi ya nane nchini Uingereza, anajivunia kuwa mtu wa kwanza kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili alipomaliza mbio maalum za INEOS1:59 Challenge kwa saa 1:59:40 mjini Vienna, Austria mwaka 2019. Kipchoge atasherehekea kufikisha umri wake 36 hapo Novemba 5.
Wanja, 36, ambaye ni seta mahiri wa klabu ya Kenya Pipeline na timu ya taifa ya Malkia Strikers, aliwabwaga Naomi Wafula (gofu), Sabrina Simader (kuteleza kwa ubao thelujini), Emily Muteti (uogeleaji), Evelyn Okinyi (mtunishaji misuli) na Hellen Obiri (mwanariadha) katika kitengo cha wanawake.
Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho na Waziri wa Michezo Amina Mohamed walishinda vitengo vya watumishi wa umma maridadi vya wanaume na wanawake, mtawalia.
Zaidi ya kura 43,000 zilipigwa kuamua washindi wa vitengo mbalimbali vilivyowaniwa katika tuzo hizo, ambazo vitengo vingi vilikuwa vya burudani.