Habari

Hatari yazidi corona ikiua 1,013

November 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

HATARI ya virusi vya corona iliendelea kudhihirika nchini Kenya huku Wizara ya Afya ikitangaza kuwa watu 1,013 walikuwa wameangamizwa na ugonjwa wa Covid-19 kufikia Jumapili.

Ripoti ya wizara ya afya ilisema kwamba, watu 17 waliuawa na ugonjwa huo ndani ya muda wa saa ishirini na nne na wengine 685 wakathibitishwa kuwa na ugonjwa huo kutokana na sampuli 4,433 zilizopimwa katika muda huo.

Kulingana na ripoti hiyo, idadi ya watu walioambukizwa virusi hivyo nchini imefikia 55,877.

Ni watu 699,790 kati ya Wakenya 49 milioni waliokuwa wamepimwa virusi hivyo kufikia jana.

Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe alisema kwamba watu 1, 271 wamelazwa katika hospitali tofauti nchini wakitibiwa na wengine 4,806 wakiendelea kuuguzwa wakiwa nyumbani.

Watu 53 wamelazwa katika wadi za wagonjwa mahtuti katika hospitali mbalimbali, 31 wakiwa wamewekwa katika mashini za kuwasaidia kupumua na 22 wakiongezewa hewa ya oksijeni.

“Kuna wagonjwa 46 wanaoongezewa hewa ya oksijeni lakini hawajalazwa katika wadi ya wagonjwa mahututi,” Bw Kagwe alisema kwenye taarifa.

Baada ya muda mrefu, kaunti ya Mombasa ilipiku Nairobi kwa kurekodi visa vingi vipya. Visa 203 vilithibitishwa katika kaunti hiyo na 202 vikathibitishwa Nairobi.

Bw Kagwe alisema kaunti za mashambani ziliendelea kusajili idadi kubwa ya maambukizi kama vile Busia 95, Nakuru 18, Kiambu 18, Bungoma 18, Kilifi 17, Kisumu 17, Embu 17, Kajiado 15, Kakamega 14, Kwale 8, Machakos 6 na Kirinyaga iliyokuwa na visa 5.

Ripoti zinasema kwamba, wadi zilizotengewa wagonjwa wa corona katika hospitali za kaunti zimeanza kujaa. Katika Kaunti ya Nairobi, shirika la Huduma za jiji (NMS) linatarajiwa kuzindua hospitali ya muda yenye vitanda 150 katika hospitali ya Mbagathi ili kukidhi idadi kubwa ya maambukizi ya corona inayoendelea kuripotiwa.

Ofisi kadhaa na mabunge ya kaunti pia zimefungwa huku watu mashuhuri wakiuawa na wengine kuthibitishwa kuwa na ugonjwa huo.

Mnamo Jumatano, Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuongoza mkutano na magavana kujadili ongezeko la maambukizi nchini. Kuna hofu kwamba huenda masharti makali yaliyolegezwa mnamo Septemba ya kuzuia msambao wa corona yakarejeshwa. Rekodi za wizara ya afya zinaonyesha kuwa, visa vimeongezeka baada ya kafyu kulegezwa, baa kufunguliwa, ibada kuruhusiwa na watu kuanza kuhudhuria mazishi na harusi.

Wanafunzi na walimu pia wameathiriwa na ugonjwa huo wiki mbili baada ya shule kufunguliwa. Wataalamu wa afya wanasema kwamba, kuna uwezekano wa maambukizi kuongezeka miezi ya Novemba na Desemba wakati wa sherehe za Krismasi na mwaka mpya.

Watu huwa wanasafiri kwa wingi mwishoni mwa mwaka. Rais Kenyatta alisema mkutano wake na magavana na wataalamu wa afya Jumatano utachunguza hali ilivyo na inavyoweza kuwa katika miezi hiyo miwili.

Mataifa mengi ulimwenguni yaliyokuwa yamefungua huduma yameanza kufunga tena baada ya maambukizi kuongezeka.