• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Apoteza nyadhifa kwa kujaa tamaa

Apoteza nyadhifa kwa kujaa tamaa

Na JOHN MUSYOKI

KIVAA, MASINGA

TAMAA ya mzee mmoja wa hapa, ilimfanya akose nyadhifa zote alizokuwa akishikilia kanisani na kijijini.

Duru zinasema kwamba mzee huyo aliteuliwa mwenyekiti wa kanisa na vilevile akachaguliwa kama kiongozi wa nyumba kumi kijijini.

Iliripotiwa kuwa licha ya mzee huyo kuwa na nyadhifa hizo zote bado alitaka kuwa kinara wa soko moja hapa.

Mzee alipandwa na kiburi na kuanza kuwadhalilisha watu wengine. Alijigamba kuwa ndiye aliyefaa kuteuliwa kuwaongoza wakazi katika kila shughuli.

“Hamfai kumchagua mtu mwingine na kuniacha. Niko tayari kufanya kazi zote mtakazonipatia. Watu wengine hapa hawawezi kuwa viongozi wenu,” mzee alijigamba.

Mdaku anaarifu kuwa watu walimsuta mzee huyo na kumtisha kwa kuwa na tamaa ya uongozi na wakaamua kumuondoa katika nyadhifa zote alizokuwa ameshikilia.

“Kwa nini unapenda kujigamba sana na vyeo hivyo vyako na hakuna kazi unayoifanya. Pia sisi tunafaa kuwa viongozi. Kwa kuwa umekuwa na tamaa ya kuongoza tutakuondoa kutoka kwa nyadhifa hizo zote kwa lazima,” jamaa mmoja alisikika akimwambia mzee.

Wakazi walikasirika mzee alipotumia lugha ya kuwadharau kwa kuwaambia hawajiwezi bila uongozi wake.

Lakini tunaarifiwa kuwa habari zilipomfikia pasta wa kanisa analoshiriki mzee huyo, aliamua kumvua uenyekiti wa kanisa mara moja.

Kwa upande mwingine, watu pia walishinikiza mzee huyo kupokonywa wadhifa wa kiongozi wa nyumba kumi.

“Hakuna aliyekuwa na imani naye tena,” alisema mdokezi.

Baada ya muda mfupi mzee huyo alipoteza nyadhifa zake zote za uongozi na hapo akagundua kwamba mtaka yote huwa anakosa yote.

You can share this post!

ODONGO: Mvutano wa wanasiasa juu ya IEBC ni njama kuidhibiti

DIMBA: Dejan, kifaa cha Juve kinachowania tuzo ya ‘Golden...