• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 2:10 PM
KAMAU: Siasa zinafaa kutujenga kama taifa si kutubomoa

KAMAU: Siasa zinafaa kutujenga kama taifa si kutubomoa

Na WANDERI KAMAU

SIASA ni mojawapo ya vumbuzi muhimu zaidi katika maisha ya mwanadamu.

Ni jambo ambalo huziwezesha jamii kuishi pamoja chini ya kanuni ama masharti fulani yaliyowekwa, licha ya tofauti ambazo huenda zikawepo miongoni mwa wanajamii.

Kanuni na mikataba hiyo huwa kama gundi ambayo huwaunganisha wanajamii husika bila tofauti kuibuka miongoni mwao.

Ikiwa kuna hali ya kutofautiana ambayo huibuka, siasa huwa na taratibu maalum za kuzisuluhisha bila kumuumiza wala kumpendelea mwanajamii yeyote.

Huo ndio msingi wa kweli katika uendelezaji wa siasa ulioanzishwa karne nyingi zilizopita.

Jamii za kikale zilizozingatia na kuendesha makubaliano ya kisiasa kwa ukweli zilipata ustawi mkubwa kiuchumi na kijamii.

Ustawi huo ulijumuisha uwezo wa kijeshi kuzivamia na kuzitawala nchi ama falme ambazo zilikosa kubuni mikakati ya kuendeleza tawala zake chini ya makubaliano yaliyopo.

Umoja wa kisiasa ndio ulizistawisha baadhi ya falme maarufu za kikale kama Roma, Ugiriki, Carthage, Misri kati ya zingine.

Kutokana na misingi thabiti ya kisiasa iliyokuwepo, athari za falme hizo zingalipo hata katika kizazi cha sasa, hasa kwenye mawanda ya historia, falsafa na utamaduni.

Hili ni licha tawala hizo kusambaratika karne nyingi zilizopita.

Katika karne ya 21, uthabiti huo ndio umeziwezesha nchi kama Uingereza, Amerika, China, Japan, Urusi kati ya zingine kuendelea kuwa zenye uwezo mkubwa zaidi kiuchumi, kijamii na kitamaduni kote duniani.

Kinaya ni kwamba, nyingi kati ya nchi hizo zinafuata mfumo wa kifalme, licha ya uwepo wa mawaziri wakuu!

Zile ambazo huwa hazifuati mkondo huo kama China, zinazingatia mfumo wa utawala wa kikomunisti, ambao huhakikisha umoja na mshikamano mkubwa miongoni mwa makundi mbalimbali yaliyopo.

Urejeleo huu bila shaka unaonyesha kuwa siasa ndizo msingi wa ustawi wa jamii na nchi yoyote duniani.

Vivyo hivyo, siasa ndicho chanzo cha jamii nyingi kusambaratika na kusahaulika kabisa, ikiwa viongozi waliopo watakosa kuziendesha kwa kuzingatia taratibu zifaazo.

Uendeshaji mbaya wa gurudumu la siasa ndio uliziangusha nchi kama Somalia, Yugoslavia, Sudan kati ya zingine.

Kutokana na tofauti za kisiasa, taifa la Somalia lilivurugika kabisa tangu 1991, baada ya aliyekuwa kiongozi wake Mohamed Siad Barre kung’atuliwa mamlakani.

Urejeleo huu unapaswa kuwa funzo kwetu kuwa siasa kamwe hazipaswi kuwa chanzo cha migawanyiko baina yetu hata kidogo, hasa kampeni za ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) na uchaguzi mkuu wa 2022 zinapoanza kushika kasi.

Badala yake, zinapaswa kuwa chemichemi ya ushindani wa kimawazo kuhusu yule anayetoa sera na mapendekezo bora zaidi katika kusuluhisha changamoto zinazotuathiri.

Huu ndio msingi tunaopaswa kukita uendeshaji wa siasa zetu. Ushindani wa umaarufu kati ya viongozi kamwe hautatufaa kwa vyovyote vile, bali utaturejesha katika giza la chuki za kikabila.

Tunafaa kutazama na kujifunza kutoka nchi kama Norway, ambapo licha ya kuzingatia mfumo wa kifalme, ni mojawapo ya mataifa yenye chumi thabiti zaidi duniani.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Mpango wa UHC katu usihujumiwe

SHINA LA UHAI: Visa vya mimba kuharibika vyaongezeka nchini