Makala

COVID-19: Ajizolea sifa kedekede kwa kutoa hamasisho

November 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na DIANA MUTHEU

KIPINDI hiki cha janga la Covid-19, George Otieno Ogallo, 43, amejizolea sifa na hata kuitwa majina kama vile ‘The Government Inspector’ na ‘Mtu wa Corona’.

Hayo yote ni kutokana na juhudi zake za kuhamasisha watu kuhusu hatari za virusi vya corona, na umuhimu wa kujikinga dhidi ya maradhi hayo.

Katika shughuli zake za kutoa hamasa kuhusu maradhi ya Covid-19, George huwa na maikrofoni na kipaza sauti chenye uzito wa kilo 17 ambacho kimebanwa vizuri katika toroli ndogo.

Kando ya toroli hiyo, amebandika picha zenye matangazo yanayoelezea kwa ufupi kumhusu, nambari zake za simu, na sheria, kanuni na masharti ya kufuata kujiepusha na corona.

Katika matangazo hayo, amesema kuwa wazazi wanafaa kuangazia na kuwa makini zaidi ili kuwaepusha watoto wao dhidi ya madhara ya maradhi ya Covid-19 ambayo ameyataja kama: mimba za mapema, matumizi ya dawa za kulevya na utekaji nyara ambao umezidi msimu wa janga hili.

Pia, kuna tangazo linalosema kuwa watu wazingatie kuvalia barakoa, wanawe mikono kwa maji safi na sabuni, pia watumie viyeyuzi.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali katika bustani ya Mama Ngina Jumamosi moja alipokuwa anafanya hamasa zake, George alisema kuwa amejitolea kuhamasisha watu kuhusu virusi vya corona, hata kama halipwi na mtu yeyote.

Alisema kuwa aliomba ruhusa kwa chifu wake na wazee wa kijiji eneo la Changamwe kabla ya kuanza shughuli hizo mnamo Aprili, mwaka huu.

“Ni muhimu wanajamii wakumbushwe kuwa janga la corona lipo na wajikinge kila wakati,” akasema George, ambaye katika shughuli hizo, utampata amevalia vinadhifu na hata kufunga tai, kuonyesha heshima anayoipa kazi yake.

Anasema kuwa akijiwasilisha mbele ya umati wa watu akiwa nadhifu, ni rahisi watu kusimama na kusikiliza ujumbe atakaotoa.

Anasema kuwa vifo vya ndugu zake wanane koutokana na magonjwa tofauti, kulimfunza kuwa ugonjwa si kitu cha kudharauliwa au kupuuzwa.

George alisema kuwa familia yao ni kubwa ambapo baba yao aliwaoa wanawake sita na kuna watoto wengi, na wengi wao wamesumbuliwa na magonjwa aina tofauti tofauti.

“Magonjwa ni kitu kibaya sana, na yanaweza kufanya mali yako ulioitafuta kwa miaka mingi iishe mara moja,” alisema huku akiongeza kuwa watu wasipuuze maagizo wanayopewa na Wizara ya Afya kuhusu jinsi wanavyoweza kujikinga na virusi hivyo, manake anaelewa uchungu wa kuwapoteza ndugu zake kwa magonjwa tofauti.

Alighadhabishwa na jinsi Wakenya wanapuuza maagizo yakuwasaidia kuwalinda na maradhi ya Covid-19.

“Tumefundishwa sana kuhusu virusi vya corona. Mbona tusifuate maagizo ili tujilinde, na mwishowe tuweze kukomesha janga hili kwa pamoja?” Akauliza.

George anasema kuwa kila siku anatenga saa mbili au tatu ili azunguke kote kote kuhamasisha watu.

“Nimezunguka Changamwe nzima, masoko yote, katika steni, uwanja wa michezo na makanisa nikihamasisha watu,” akasema George ambaye kabla ya janga hili alikuwa akitoa mafunzo kwa vijana katika sekta ya huduma za hoteli.

George Otieno Ogallo akimpa barakoa mwanamke mwenye ulemavu barabarani. Picha/ Diana Mutheu

George ambaye ni baba wa watoto wanne anasema kuwa ametumia takriban Sh45,000 kununua vifaa anavyovitumia katika mpango huu na anaamini kuwa juhudi zake zitazaa matunda.

Alisema kuwa akipata msaada wa aina yoyote kutoka kwa serikali ya kaunti au msamaria mwema, atanunua pikipiki itakayomwezesha kusafiri katika maeneo yote ya Kaunti ya Mombasa.

Hata hivyo, anasema kuwa mara kadhaa amekataliwa na hata kupuuzwa katika sehemu tofauti tofauti.

“Nikiifanya kazi hii, ningependa kuwashukuru marafiki zangu walionisaidia. Hata hivyo, si kila mtu ataona umuhimu katika mambo unayoyafanya. Lakini, nitaendelea kung’ang’ana kwa sababu ninajua kuwa ujumbe ninaousambaza utaweza kuisaidia jamii yangu,” akasema huku akiahidi kuwa atazidi kutoa hamasisho kwa kuwa janga hili limerejea kwa vishindo na linatikisa nchi.

“Nitazidisha shughuli hizi sana. Naamini bado Wakenya wanahitaji kukumbushwa kuwa virusi vya corona vipo na vinaua. Zaidi, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema kuwa polisi hawawezi kutulinda sote, ila jukumu ni la kila mwananchi,” akasema George.

Anawashauri Wakenya wasiwe wepesi wa kupuuza maagizo, ila wafuate hatua zote za kujikinga waepuke maambukizi ya virusi vya corona.

“Tukifuata maagizo, tutamaliza maradhi ya Covid-19,” akasema.