• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 9:50 AM
MATHEKA: Tusikubali BBI ipokonye mahakama uhuru wake

MATHEKA: Tusikubali BBI ipokonye mahakama uhuru wake

Na BENSON MATHEKA

RIPOTI ya Mpango wa Maridhiano (BBI) imezua migawanyiko tangu ilipozinduliwa wiki jana na hakuna dalili za pande zinazotofautiana kupatana.

Hii ni kwa sababu wanaoiunga mkono wamesema kwamba hakuna nafasi ya kuibadilisha hata ingawa wakati wa kuizindua, vinara wa mchakato huo- Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga- walisema maoni ya Wakenya yanakaribishwa ili kuimarisha ripoti hiyo.

Ni kawaida ya wanasiasa kutofautiana kuhusu masuala kama haya lakini kuna haja ya kutofunga milango ya mazungumzo kwa kuwa mabadiliko yanayopendekezwa yataathiri Wakenya.

Ripoti hiyo ina mengi mazuri na wengi wanakubali hivyo. Hata hivyo, mazuri yaliyomo yanaweza kuharibiwa na moja mbaya kama kujaribu kuondoa uhuru wa mahakama.

Ni bayana kuwa Wakenya huwa wanakimbia mahakamani kutafuta haki wanapokadamizwa na serikali na maafisa wake. Hii ndiyo sababu walioandika katiba ya 2010, waliimarisha uhuru wa mahakama kwa kuhakikisha majaji na wafanyakazi wa idara hiyo sio vibaraka wa rais.

Kwa kufanya hivi, Tume ya kikatiba ya Huduma ya Mahakama (JSC) ilibuniwa na kutwika jukumu la kusimamia mahakama ikiwa ni pamoja na kuajiri majaji kuanzia Jaji Mkuu.

Hatua hii haikufurahisha viongozi wa kisiasa ambao wanahisi kwamba kwa kuwa huru, mahakama imekuwa ikihujumu serikali kuu.

Kauli za kupotosha zimetolewa na wanasiasa kuhusu utendakazi wa mahakama na pendekezo la ripoti ya BBI kwamba kubuniwe afisa wa kupokea malalamishi kuhusu mahakama na majaji atakayeteuliwa na rais na kuketi katika JSC, linaonekana kuwa njama za kuhujumu uhuru huo.

Ni pendekezo ambalo limepingwa na mawakili na baadhi ya viongozi na kwa kusema kuwa milango ya kujadili ripoti hiyo imefungwa ni kudhibitisha kuna njama za kupokonya mahakama uhuru wake.

Kupendekeza rais kuteua afisa kuketi katika JSC, ni sawa na kuteka uhuru wa mahakama na kufanya majaji kutokuwa na uhuru wa kutekeleza majukumu yao.

Ni kurejesha Kenya enzi za katiba ya zamani iliyobadilishwa 2010 ambapo watu wenye ushawishi walikuwa wakitumia mahakama kukadamiza wapinzani wao.

Majaji waliokuwa wakiteuliwa na rais walikuwa wakitoa maamuzi kufurahisha mwajiri wao na sio kwa haki. Pendekezo hili linalenga kuhakikisha kuwa rais atakuwa akishawishi maamuzi yote ya JSC.

Kwa kuwa tume hiyo ndiyo huwa inaajiri majaji, hii itamaanisha kuwa watakaoajiriwa watakuwa wale anaopenda rais.

Inafaa kukumbukwa kwamba kuna majaji 41 ambao rais amekataa kuapisha akilaumu JSC kwa kuajiri watu ambao hawafai. Rais amekuwa akilaumu mahakama kwa kuhujumu ajenda za serikali. Inafaa kukumbukwa kuwa wabunge wamekuwa wakilaumu mahakama kwa maamuzi yasiyowapendelea.

Haya yote yanaonyesha kuwa wanasiasa wana kisasi na mahakama na kulingana nao, kuna haja ya kuikata miguu kupitia mchakato kama BBI.

Kama nilivyotangulia kusema, mengi mazuri yaliyo katika ripoti ya BBI yanaweza kutiwa ndoa na kupokonya mahakama uhuru wake.

Kupitisha pendekezo kama hilo ni sawa na Wakenya kujitia kitanzi. Tunaposhangilia ripoti hii, tunafaa kukumbuka kuwa ni katika mahakama pekee ambapo tunaweza kukimbilia tukinyimwa haki na bunge na serikali kuu.

You can share this post!

TAHARIRI: Mikutano ya kisiasa heri iwe marufuku

WANGARI: Vyombo vya habari Magharibi vikome kuisawiri...