Manchester City yapepeta Olympiakos na kujipa motisha ya kukabili Liverpool katika mechi ijayo ya EPL
Na MASHIRIKA
GABRIEL Jesus alirejea uwanjani kwa matao ya juu na kusaidia Manchester City kuwapepeta Olympiakos 3-0 katika mechi ya Kundi C ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 3, 2020.
Ushindi huo uliendeleza rekodi ya asilimia 100 ya Man-City katika kampeni za msimu huu baada ya kusajili ushindi katika michuano mitatu ya hadi kufikia sasa kundini.
Man-City walichukua uongozi wa mechi hiyo kupitia kwa sajili mpya Ferran Torres kunako dakika ya 12 kabla ya Jesus kupachika wavuni goli la pili katika dakika ya 81. Kiungo Joao Cancelo alitokea benchi katika kipindi cha pili na kufungia Man-City ya kocha Pep Guardiola bao la tatu katika dakika ya 90.
Mchuano huo dhidi ya Olympiakos ya Ugiriki ulikuwa wa kwanza kwa Jesus kuwajibishwa kambini kwa Man-City tangu Septemba 21 alipopata jeraha la goti.
Hii ni mara ya tatu kwa Man-City kufunga mabao matatu katika soka ya UEFA chini ya kipindi cha wiki tatu zilizopita. Hadi walipowachabanga Olympiakos, Man-City walikuwa wakijivunia kushinda FC Porto ya Ureno na Olympique Marseille kutoka Ufaransa.
Ina maana kwamba Man-City kwa sasa wanahitaji alama moja pekee kutokana na mechi ijayo ya marudiano dhidi ya Olympiakos nchini Ugiriki ili kujikatika tiketi ya kuingia hatua ya 16-bora ya UEFA msimu huu wa 2019-20.
Kocha Guardiola ameeleza kwamba ushindi uliosajiliwa na masogora wake dhidi ya Olympiakos utawapa motisha zaidi ya kuwabwaga Liverpool katika mechi ijayo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) itakayowakutanisha ugani Etihad mnamo Novemba 8, 2020.
Mbali na Jesus na Torres walioshirikiana vilivyo na kuwatatiza mabeki wa Olympiakos, mchezaji mwingine wa Man-City aliyetamba zaidi katika mechi ya Novemba 3 ugani Etihad, Uingereza ni kiungo Kevin De Bruyne aliyeshirikiana pakubwa na chipukizi Phil Foden.