Wakili Gicheru kuishi ‘vizuri’ katika seli ICC
Na VALENTINE OBARA
WAKILI Paul Gicheru, anayedaiwa kuvuruga mashahidi wa kesi iliyomkumba Naibu Rais William Ruto katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ataishi kizuizini The Hague, Uholanzi kwa muda.
Wakili huyo alijisalimisha kwa polisi wa Uholanzi Jumatatu, na akafikishwa kizuizini Jumanne kwa mujibu wa mahakama hiyo.
Mahakama ingali inasubiriwa kutoa mwelekeo kuhusu jinsi kesi yake itakavyoendeshwa, ikiwemo kama ataruhusiwa kuwa huru kesi ikiendelea ama atatakikana kufungiwa seli.
“Mshukiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni. Mahakama itahitajika kumtambua rasmi, kisha kuweka tarehe ambapo majaji wataanza kusikiliza pande zote za kesi ili kuamua kama kesi itaendelezwa mbele,” ikasema taarifa kutoka ICC mnamo Jumatano usiku.
Hata hivyo, maisha ndani ya seli za ICC si magumu jinsi ilivyo katika seli za humu nchini.
Kizuizi cha washukiwa wa ICC kiko ndani ya jela ya Uholanzi viungani mwa The Hague.
Kuzuizi hicho kinachosimamiwa na Msajili wa Mahakama wa ICC huruhusu washukiwa kupokea huduma za hali ya juu ambazo zinatimiza sheria za kimataifa kuhusu hali za binadamu, kulingana na maelezo kutoka kwa mahakama hiyo.
“Ratiba ya kila siku katika kizuizi hicho huruhusu wafungwa kupata hewa safi, muda wa kucheza michezo ya spoti au kunyoosha misuli. Wanaruhusiwa kusoma vitabu, magazeti na kutazama televisheni katika maktaba,” inaeleza ICC.
Vile vile, akiwa kizuizini, Bw Gicheru atakuwa na haki ya kutumia kompyuta iliyounganishiwa intaneti kuandaa kesi yake.
Kwa wafungwa ambao hawana ujuzi wa kutumia tarakilishi, mahakama huwafadhili kupokea mafunzo.
Ndani ya seli, kila mfungwa ana kompyuta ambayo mtandao wake umeunganishwa kwa kompyuta nyingine moja pekee ndani ya mahakama. Tarakilishi hiyo inaweza kutumiwa na mawakili wake kumtumia stakabadhi za kesi ili ajifahamishe nazo.
“Mawasiliano hayo hayawezi kufuatiliwa na mtu mwingine yeyote, wakiwemo wafanyakazi wa kizuizi,” ICC inasema.
Kuhusu masuala ya kidini, Bw Gicheru ataruhusiwa kutembelewa na mhubiri au kiongozi yeyote atakaye wa kidini anayetaka. Kuna sehemu maalumu iliyotengwa kwa shughuli za kidini kati ya mfungwa na mhubiri.
Vile vile ICC itamruhusu mshukiwa huyo kutembelewa na jamaa zake akiwemo mkewe, na mahakama itajitolea kumsaidia mke wake kutimiza ziara hiyo akitaka.
Ijapokuwa mahakama hiyo inasema huwapa wafungwa lishe bora, kila mfungwa huruhusiwa kujipikia jinsi anavyotaka kwani huenda wapishi hawafahamu jinsi ya kupika vyakula vya kitamaduni.
Kizuizi cha ICC huwa hakitumiwi kufunga watu waliohukumiwa, ambao huhamishwa hadi katika magereza ya mataifa yanayoshirikiana na mahakama hiyo. Agizo la kukamatwa kwa Bw Gichuru lilitolewa mwaka wa 2015.
Wakenya wengine ambao wanatakikana kukamatwa na kufikishwa ICC kwa madai ya kushawishi mashahidi kujiondoa katika kesi za ghasia zilizokumba nchi baada ya uchaguzi wa 2007, ni Walter Barasa na Philip Kipkoech Bett.