AKILIMALI: Teknolojia ya mitego maalum yamsaidia kukabili wadudu waharibifu katika miembe
Na SAMMY WAWERU
KAMBITI, eneobunge la Maragua, Kaunti ya Murang’a ni kati ya maeneo tajika katika uzalishaji wa maembe dodo.
Katika shamba la John Ndung’u lenye ukubwa wa ekari mbili na linalositiri takriban miembe 180, tunampata akiikagua, huku ikiwa inachana maua na baadhi kutunda.
Kwenye kila mti, hutakosa kutazama mikebe ya rangi ya manjano na mingine mieupe, iliyofunikwa kwa mikebe inayowiana au vifuniko vya mviringo.
Mkulima huyo anafichua kwamba, mikebe hiyo ni mitego maalum yenye madhumuni kuteka na kunasa wadudu waharibifu katika miti ya maembe.
Ndung’u aliingilia kilimo cha maembe 1998, baada ya kuwa katika ukuzaji wa mahindi, maharagwe na mihogo kwa muda mrefu, mimea anayotaja hulimwa sana eneo hilo. “Nilianza na miti 10 ya maembe asilia, niliyoipanda katika nusu ekari,” anadokeza, akisema kwamba baadaye aliiimarisha kwa kupandikiza na ya kisasa.
Alipoona maembe yana mapato ya kuridhisha, Ngung’u anasema aliongeza nusu ekari zaidi, ikawa anayakuza kwenye ekari moja. “Hatimaye nilijipata ninayalima katika ekari mbili, kutokana na msukumo wa faida,” anaelezea.
Sawa na matunda mengine, mkulima huyo anasema hayakukosa changamoto zinazoshuhudiwa mara kwa mara, kama vile shambulio la wadudu na magonjwa, na pia nyakati zingine soko kumpiga chenga.
Kulingana na Ndung’u, mambo yalianza kuenda mrama mwaka wa 2006, nzi wa matunda waliporipotiwa kwa mara ya kwanza nchini. “Ni wadudu waharibifu sana. Hawaruhusu maembe kukua na kukomaa ipasavyo, nusra yazime ndoto zangu,” anasema mkulima huyo.
Nzi wa matunda, hawashambulii maembe pekee, hata katika matunda mengine.
“Kando na matunda, pia hayasazi maboga (malenge). Pindi wadudu hao wanapoingia katika shamba la matunda, ikiwa hutachukua hatua za mapema kuwadhibiti usitarajie kuvuna chochote,” anaonya Samson Nduati, mtaalamu.
Aidha, wadudu hao ni wa rangi ya kahawia au ya ngozi. Hutoboa mashimo kwenye matunda, wanaingia, na kuyageuza makao ya uzazi, mdudu mmoja wa kike akikadiriwa kutaga mayai 500 yanayoangaliwa chini ya saa 24 – 30. Nduati anasema hilo hufanya kuwa vigumu kuwadhibiti.
Kilele kinakuwa matunda kuiva kabla ya kukomaa, yaani yakiwa yangali machanga na madogo, na kulingana na Ndung’u baadhi huanza kuanguka kiholela.
Anafafanua kwamba, maembe yaliyoathirika huwa kali na kudondoa juisi, suala linalochangia wateja kuyakataa. Kimsingi, yanakataliwa sokoni.
Nzi wa matunda hukita kambi kwenye miti inapoanza kuchana maua hadi steji ya kutunda. “Dalili zingine za matunda yaliyoshambuliwa ni kuwa na madoadoa meusi, wadudu hao wakiwemo ndani,” Ndung’u anadokeza, akiongeza kwamba athari hizo pia hushusha ubora au hadhi ya mazao.
Hasara
Wakati wa mahojiano na Akilimali, Ndung’u alisema alikuwa akigharimika kukabili wadudu hao waharibifu, kiasi cha kukadiria hasara kila msimu. “Gharama ya kemikali kukabili wadudu si mchezo, ni ghali mno. Isitoshe, matunda yaliyozalishwa kwa kutumia dawa zenye kemikali hunuka, na wanunuzi wengi hawayakubali kwani wanataka yaliyokuzwa kwa kuzingatia mfumo wa kilimohai,” anafafanua.
Fauka ya hayo, mazao yaliyopuliziwa dawa zenye kemikali si salama kiafya kwa walaji, Ndung’u pia akihoji kemikali huua nyuki wanaosaidia katika uchavushaji mtambuka (cross pollination) wa mbegu za kiume kwenye miti ya maembe.
Pandashuka hizo, anasema aliweza kuziangazia mwaka wa 2017, matumizi ya mitego maalum kuteka na kunasa wadudu ilipojiri.
Hata ingawa mfumo wa mitego hiyo si asilimia 100 kwa 100, anathibitisha kwamba ni nadra kutumia dawa zenye kemikali kukabili nzi weupe na wadudu wengineo waharibifu katika uzalishaji wake wa maembe.
Dalili za miembe kuanza kuchana maua zinapobisha hodi, mitego hutiwa kemikali inayonukia, kuua wadudu. Kemikali hizo zimegawanywa kwa makundi mawili; ‘Bactrolure’ inayoua wadudu wa kiume, na ‘Torula’ ya kukabili wale wa kike.
Mtaalamu Samson Nduati anasema wadudu wa kiume ndio lengo kuu, ili kusitisha ujamiishaji. “Wadudu wa kiume wakiuawa, hakutakuwa na ujamiishaji hivyo basi uzazi hautaendelea,” anaelezea mdau huyo.
Mbali na kutiwa kemikali, mikebe inayotumika kama vifunikio na yenye mashimo mawili wanamoingilia wadudu, huwekwa molasi ambayo huwavutia.
Mitego ina ndoano ya nyaya kuininginiza kwenye matawi ya miti. “Wadudu huanza kuingia wakitafuta harufu inayonukia. Dawa iliyowekwa huwaangamiza, na wanaotoka hawafanikiwi kuishi,” Ndung’u anafafanua, akiridhia ubunifu wa mitego hiyo inayotengenezwa na kampuni ya Techno Serve.
Aidha, mtego mmoja una uwezo kunasa takriban wadudu 1, 000 kwa siku.
Mkulima huyo anaungama matumizi ya teknolojia hiyo ya mitego imeshusha gharama ya ukuzaji wa maembe kwa asilimia 75, akilinganisha na gharama ya dawa za kupulizia miti na matunda kukabili wadudu.
Mtego mmoja unauzwa Sh350, na humhudumia kipindi cha muda wa miaka minne mfululizo. “Dawa katika kila mtego haizidi Sh250, na huongezwa baada ya miezi mitatu,” Ndung’u asema.
Mfumo huo unasifiwa katika kuafikia kilimohai, mtaalamu Nduati akisema mkulima anaweza kujiundia mitego kwa kutumia mikebe ya plastiki iliyotupwa, hatua ambayo pia inasaidia kuhifadhi mazingira.
Miembe ya Ndung’u ni iliyoimarishwa kwa njia ya kupandikiza, na ikizingatiwa kuwa amekumbatia mfumo wa kilimohai, anasema mazao yake huwa na ushindani mkuu katika masoko mbalimbali Nairobi na viunga vyake, pia akifichua ana wanunuzi nje ya nchi.
Changamoto inayomzingira, ni wakulima wenza hususan majirani na ambao hawajakumbatia mfumo wa mitego hiyo. Analalamika kuwa mashamba yao ni pango-fichio la wadudu wanaotoroka kwake.
Hukuza maembe aina ya Tommy, Kent na Sabine, na kwa mujibu wa maelezo yake wakati wa mahojiano, aliashiria kuwa huingiza mapato ya kuridhisha.
Kwa kawaida, nyuki huvutiwa na harufu ya kunukia na juisi ya maua, na dalili ya maembe kuanza kutunda ni kuchana maua. Sawa na miti mingine inayochana maua, kipindi cha miembe kuyachana, hualika mamia, mamia ya maelfu ya nyuki, iwapo si mamilioni.
Ni wadudu wenye manufaa na tija chungu nzima na ambao wakati alikuwa akitumia dawa zenye kemikali kuua wadudu waharibifu kwa maembe, nyuki pia walikuwa wakiangamia.
Mfumo wa mitego ya kipekee, inayotiwa dawa na molasi kukabili nzi wa matunda, Ndung’u anasema umemuwezesha kufuga nyuki, na kujipa pato la ziada kupitia uvunaji wa asali.