Michezo

Manchester United waaibishwa na Istanbul Basaksehir FK kwenye gozi la UEFA nchini Uturuki

November 5th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

WANASOKA wa Manchester United waliondoka uwanjani wakiinamisha vichwa kwa aibu baada ya kupokezwa kichapo cha 2-1 na Istanbul Basaksehir FK ya Uturuki kwenye mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 4, 2020.

Basaksehir walioanzishwa mnamo 1990 walitia kapuni taji la Ligi Kuu ya Uturuki (Turkish Super Lig) kwa mara ya kwanza msimu uliopita wa 2019-20.

Hadi walipowaaibisha Man-United, Basaksehir hawakuwa wamejivunia alama yoyote wala kufunga bao kwenye mechi mbili za ufunguzi wa kundi lao kwenye UEFA.

Utepetevu kwenye safu ya nyuma ya Man-United uliruhusu fowadi wa zamani wa Chelsea na Newcastle United, Demba Ba kuwafungulia Basaksehir ukurasa wa mabao kunako dakika 12 baada ya kumzidi maarifa Dean Henderson.

Bao hilo liliwapa Basaksehir motisha zaidi na nusura wafunge la pili katika dakika ya 15 baada ya Deniz Turuc kumzidi ujanja kiungo Juan Mata kabla ya kumwandalia Edin Visca krosi safi iliyojazwa wavunia mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Man-United waliokuwa wageni kwenye mechi hiyo walipata matumaini ya kurejea mchezoni baada ya kufungiwa goli na Anthony Martial aliyeshirikiana vilivyo na beki Luke Shaw dakika mbili kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha kwanza kupulizwa.

Kichapo cha 6-1 ambacho Man-United walipokezwa na Tottenham Hotspur kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Oktoba 2020 kilitarajiwa kuwazamisha kabisa.

Ingawa hivyo, waliweka kando maruerue ya kichapo hicho na wakasajili ushindi kwenye michuano mitatu mfululizo na kusajili sare moja kabla ya kuwaendea Basaksehir nchini Uturuki.

Man-United walishuka dimbani dhidi ya Basaksehir wakipigiwa upatu wa kujinyanyua baada ya kupokezwa kichapo cha 1-0 na Arsenal kwenye EPL mnamo Novemba 1, 2020 uwanjani Old Trafford.

Ingawa ushindi wa Basaksehir unatarajiwa sasa kumtia kocha Ole Gunnar Solskjaer presha zaidi ya kutafuta beki wa kati katika muhula mfupi ujao wa uhamisho wa wachezaji mnamo Januari 2021.

Mechi iliyowakutanisha Man-United na Basaksehir ilikuwa ya kwanza kwa kipa Henderson ambaye ametegemewa zaidi kwenye Carabao Cup msimu huu kunogesha kwenye UEFA.

Basaksehir wangalifunga bao la tatu mwishoni mwa kipindi cha pili ila fowadi Danijel Aleksic akashuhudia kombora lake likidakwa kirahisi na Henderson.

Mbali na Martial, mwanasoka mwingine aliyeridhisha zaidi kambini mwa Man-United ni kiungo Bruno Fernandes ambaye alimtatiza pakubwa kipa Mert Gunok aliyefanya kazi ya ziada na kupangua fataki za Paul Pogba na sajili moya Edinson Cavani.

Man-United waliingia kwenye gozi hilo wakijivunia kusajili ushindi kwenye mechi mbili za ufunguzi kundini baada ya kuwapiga Paris St-Germain (PSG) na RB Leipzig.

Baada ya kupoteza mechi mbili zilizopita, Man-United kwa sasa wana ulazima wa kusajili ushindi dhidi ya Everton katika mechi ya EPL itakayowakutanisha uwanjani Goodison Park mnamo Novemba 7, 2020.

Kichapo kutoka kwa Basaksehir kilitamatisha rekodi nzuri ya kutoshindwa kwa Man-United katika jumla ya mechi 19 zilizopita ugenini.

Hadi walipopigwa na mabingwa hao wa Uturuki, mara ya mwisho kwa Man-United kushindwa ugenini ni katika mechi iliyowakutanisha na Liverpool ligini mnamo Januari 2020.