Michezo

Injera, Amonde matumaini tele kikosi chao cha SFX10 kitatwaa ufalme wa raga ya World Tens Bermuda

November 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MWANARAGA nyota wa timu ya taifa ya Shujaa, Collins Injera, amesema kufaulu kwa kikosi cha SFX10 kuingia kwenye kivumbi cha dunia cha wanaraga 10 kila upande nchini Bermuda – japo kwa kuchelewa – kumewaacha na kiu zaidi ya kutia kapuni ubingwa wa taji hilo.

SFX10 walianza kampeni zao wiki moja baada ya mwanzo wa kampeni hizo kutokana na tukio kwamba mwanaraga mmoja wa kikosi chao alipatikana na virusi vya corona. Hata hivyo, walitawala mechi zao zote tatu mnamo Novemba 2, 2020 kwa kuwapiga Rhinos 24-5, Phoenix 30-0 na Miami Sun42-5.

“Usalama lilikuwa suala muhimu kabla ya kampeni kuanza. Sasa tuna kiu ya kutwaa ufalme wa kivumbi hicho. Tunajivunia kikosi kizuri chenye wachezaji mahiri walio na tajriba pevu na uzoefu mpana,” akasema Injera.

Hata hivyo, ameonya kwamba huenda kampeni hizo za IPL World Tens zikatawaliwa na ushindani mkali zaidi kuanzia hatua ya mwondoano.

“Nadhani kikosi chetu kimewaamshia wapinzani motisha zaidi. Mambo yatakuwa magumu na mazito zaidi tukiingia robo-fainali. Kivumbi hiki kinajivunia huduma za wachezaji bora zaidi duniani, nasi tuna kiu ya kuibuka washindi,” akaongeza.

Kikosi cha SFX10 kinajivunia pia maarifa ya mchezaji Cecil Afrika wa timu ya taifa ya Afrika Kusini almaarufu Springbok Sevens na mwanaraga matata Luke Treharne wa Wales.

Mbali na Injera, wanaraga wengine wa humu nchini ambao wananogesha kivumbi cha World Tens wakivalia jezi za SFX10 ni Monate Akuei, Willy Ambaka, Oscar Ouma, Oscar Dennis na nahodha wa Shujaa, Andrew Amonde. Kikosi cha SFX 10 kutoka Cape Town, Afrika Kusini kinanolewa na mwanaraga wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Frankie Horne.

Amonde ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Shujaa amesema mechi za World Tens nchini Bermuda zinatarajiwa kuwapa jukwaa mwafaka zaidi la kujiandaa kwa michezo ijayo ya Olimpiki jijini Tokyo, Japan mnamo Julai 2021 hasa baada ya kusitishwa kwa duru nne za Raga ya Dunia mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20.

“Hadi tulipoanza kushiriki kivumbi cha World Tens nchini Bermuda, hatukuwa tumeshiriki mechi yoyote kwa zaidi ya miezi saba. Kipute hiki kinatupa fursa ya kujifunza mengi kutoka kwa baadhi ya wanaraga maarufu zaidi duniani na uzoefu huo utatupa nafasi ya kutamba zaidi kwenye Olimpiki zijazo,” akasema Amonde.

Mechi za raundi ya kwanza ya kipute cha World Tens nchini Bermuda zilianza Oktoba (24-25) kabla ya zile za raundi ya pili kutandazwa kati ya Oktoba 31 na Novemba 1. Fainali za kivumbi hicho kitakachoshirikisha vikosi saba ni Novemba 7, 2020 uwanjani National Sports Centre.

Kipute cha World Tens kinaandaliwa kwa mfumo wa ligi za kawaida ambapo kila kikosi kitacheza na kingine mara mbili kufikia mwisho wa wikendi tatu zijazo.

Mbali na kikosi cha SFX 10 kutoka Cape Town, Afrika Kusini, washiriki wengine ni Asia Pacific Dragons (Singapore), Phoenix (Mashariki ya Kati), London Royals (London), Miami Sun (Florida), Rhinos (California Kusini) na Ohio Aviators (Columbus).

“SFX 10 kinajivunia wanaraga wenye tajriba pevu na uzoefu mkubwa kimataifa. Tuliwajumuisha wanaraga wa kikosi cha Shujaa kutoka Kenya kwa sababu taifa hilo ni mojawapo ya mataifa ambayo ni ngome ya wanaraga stadi duniani sawa na New Zealand, Fiji, Amerika na Afrika Kusini,” akasema Horne.