• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
DAISY: Ndoa ni kwa hiari ya mtu, wanawake wasihukumiwe

DAISY: Ndoa ni kwa hiari ya mtu, wanawake wasihukumiwe

Na LUCY DAISY

KITAMADUNI, wanaume waliruhusiwa kuwaoa wake wengi.

Wakati ule mwanaume aliyekuwa na mali nyingi alitarajiwa kuwa na wake kadhaa kwani alikuwa na uwezo wa kuwatunza.

Nao wanawake walionekana kama mali ya waume wao, hivyo basi mwanamume aliyekuwa na wake wengi alionekana kuwa mwenye mali nyingi. Wakati ule watu wengi walifuata utamaduni wala hawakuwa wamejua mambo ya kidini.

Baada ya dini kuingia Afrika, dini ya Kikristo haikuruhusu jambo hili, huku waislamu wakiruhusiwa kuoa wake hadi wanne.

Dini ya Kikristo inashikilia imani kuwa mwanamume anafaa kuoa mwanamke mmoja tu, hasa kama atafanya harusi ya kanisani.

Biblia inazungumzia Adamu na Hawa ambao walikuwa mke na mume; na hivyo Wakristo wana imani kuwa mume anafaa kuoa mke mmoja tu.

Hata hivyo, siku hizi Wakenya wengi wameanza kupiga darubini masuala ya dini, hasa Wakristo, na wanaonelea ni vyema kurudia desturi zao za kitamaduni.

Wengi wao wanasema dini ililetwa Afrika na wazungu na ilikuja kudunisha imani za kitamaduni za Kiafrika. Ndiposa wengi siku hizi wameamua kurejelea kuabudu miungu yao ya kitamaduni.

Ni juzi tu ambapo mwimbaji wa nyimbo za Kikuyu kwa jina Muigai Njoroge aliweka picha mtandaoni akiwa na wake zake wawili wakionekana kuwa wenye furaha wote. Mwimbaji huyu anajulikana kwa kufuatilia imani ya kitamaduni; anaamini kuwa kama watamaduni wengine, ni sawa kuoa wake wawili au zaidi.

Wengi walimsuta Muigai kwa hili, lakini wengine pia walimtaja kuwa muungwana kwa kuoa wake wawili na kuwapenda wote na pia kuwaonyesha kuwa wanafaa kuishi kwa amani bila chuki. Wake hawa walionekana wenye furaha.

Kwa maoni yangu si dhambi kwa mwanamume kuoa wake wawili au hata zaidi, iwapo ni kwa hiari yao na hakuna aliyelazimishwa. Pia, iwe hawahisi kana kwamba wanadhulumiwa kwa njia yoyote ama kudunishwa.

Wanawake wana haki ya kuamua kuishi maisha wanayotaka bila kusutwa na yeyote. Hivyo, iwapo wanawake hao ndio wamechagua maisha hayo ya ndoa bila kulazimishwa na yeyote, tena wana furaha, basi hawafai kuhukumiwa na yeyote.

Hata hivyo, kama tutaendelea kuzungumzia usawa wa kijinsia maoni yangu ni kwamba wanawake pia wana haki ya kuamua kuwa na waume zaidi ya mmoja kama vile wanaume wanaruhusiwa kuoa wake wengine.

Iwapo ni mali mtu anahitaji ili kuoa wake wengi, wanawake siku hizi wana mali pia, wana uwezo wa kijitosheleza na kuchunga familia zao vyema zaidi.

Kwa hivyo, kama mitara itakubalika nchini, basi wanawake wanaoamua kuwa na waume zaidi ya mmoja pia waache kuhukumiwa.

Sote tuko sawa na kila mja ana haki ya kuishi atakavyo mradi asiwe anahatarisha maisha ya yeyote.

Jamii haina budi kuacha kuwahukumu wanawake vibaya kwa kitendo ambacho kikifanywa na wanaume wanasifiwa.

You can share this post!

Maandamano Amerika Trump akipinga matokeo ya kura

KAMAU: Ni kosa kutowatambua mashujaa wetu nchini