• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
Barcelona kuwauza wanasoka watano baada ya kulemewa kifedha

Barcelona kuwauza wanasoka watano baada ya kulemewa kifedha

Na MASHIRIKA

MATATIZO ya kifedha yanayotishia kulemaza uthabiti wa Barcelona yamesukuma kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kufichua azma ya kuwatia mnadani wanasoka watano mnamo Januari 2021 ili kupunguza gharama ya matumizi ya pesa.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo, Barcelona watapania kuwauza wachezaji Ousmane Dembele, Martin Braithwaite, Carles Alena, Junior Firpo na Samuel Umtiti.

Kufikia sasa, kikosi hicho kinachonolewa na kocha Ronald Koeman tayari kimeagana na masogora Arthur Melo aliyetua Juventus, Ivan Rakitic aliyejiunga na Sevilla, Arturo Vidal aliyesajiliwa na Inter Milan, Nelson Semedo aliyeyoyomea Wolves na Luis Suarez aliyepata hifadhi kambini mwa Atletico Madrid.

Gazeti la Mundo Deportivo limesisitiza kwamba wachezaji Marc-Andre ter Stegen, Gerard Pique, Frenkie de Jong, Antoine Griezmann, Lionel Messi na chipukizi Ansu Fati ndio wa pekee ambao wana uhakika wa kusalia kambini mwa Barcelona kwa muda mrefu ujao.

Koeman ameambiwa na usimamizi wa Barcelona kupunguza wanasoka wa gharama kubwa ambao hawahitajiki kwa sasa kambini mwake ili kutoa fursa ya kusukwa upya kwa kikosi hicho kuanzia mwisho wa msimu huu wa 2020-21.

Kati ya wachezaji ambao Koeman, 57, anatarajiwa kuwashawishi Barcelona kusajili mwishoni mwa muhula huu ni fowadi Memphis Depay wa Olympique Lyon na Eric Garcia wa Manchester City.

Kusajiliwa kwa wawili hao mwanzoni mwa msimu huu wa kulitatizwa na janga la corona ambalo limeathiri pakubwa Barcelona ambao wamekadiria hasara ya Sh12 bilioni tangu mwanzoni mwa Machi 2020.

Dembele huenda akatua kambini mwa Manchester United iwapo kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kitaambulia pakavu kwa mara nyingine katika juhudi za kujinasia huduma za kiungo Jadon Sancho kutoka Borussia Dortmund.

Dembele ambaye kwa sasa anauzwa kwa Sh6.3 bilioni pekee, alitua ugani Camp Nou mnamo 2017 baada ya kuagana na Dortmund kwa kima cha Sh17 bilioni.

Kwa upande wake, Umtiti ambaye ni raia wa Ufaransa, anahusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua Arsenal au Man-United. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 bado hajawajibishwa katika mechi yoyote msimu huu kutokana na jeraha la goti.

Ujio wa Depay utatamatisha kipindi cha kuhudumu kwa fowadi raia wa Denmark, Braithwaite, 29, kambini mwa Barcelona ambao pia watakuwa radhi kuwauza viungo Carles Alena, 22, na Junior Firpo, 24.

You can share this post!

John Kiplangat tayari kwa makala ya saba ya mbio za Deaf...

Arteta atarajia makuu zaidi kutoka kwa Nicolas Pepe