Makala

AKILIMALI: Mwalimu anayetambua umuhimu wa ufugaji na kilimo 

November 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMMY WAWERU

JOHN Mwangangi amekuwa mwalimu kwa zaidi ya miaka 30, chini ya tume ya kuwaajiri walimu nchini ndiyo TSC.

Ni mwalimu nguli wa Somo la Kiswahili, ambapo kwa sasa anafanya kazi katika Shule ya Msingi ya Kangocho iliyoko Karatina, Kaunti ya Nyeri.

Kando na kuwa mwalimu, Mwangangi, 59, ni mfugaji hodari wa kuku na ndege wa umaridadi nyumbani kwake Karatina.

Huku akiwa amesalia na mwaka mmoja pekee kuweka chaki chini, mwalimu huyo anasema hakuna jambo muhimu kama kutayarisha jukwaa la maisha ya usoni, baada ya kustaafu, yatakavyokuwa.

“Ndiyo, eneo la Kati ni maarufu katika shughuli za kilimo, na ndicho nimewekeza kwacho kiwe afisi yangu baada ya kustaafu, nimesalia na mwaka mmoja pekee majina yangu yaondolewe kutoka katika orodha ya TSC,” anasema Mwangangi.

Baadhi ya watumishi wa umma, wakiwa kazini huponda raha na kusahau ajira ni ya muda tu, kustaafu kwaja watakapofikisha miaka inayohitajika.

Isitoshe, uhakika wa kudumu katika ajira si asilimia 100 kwa 100, hivyo basi ni muhimu kujipanga na mradi kujiendeleza kimaisha na pia kuwa na pato la ziada.

Huku Mwangangi akiwa mwalimu mwenye tajiriba ya kipindi cha muda mrefu, kuingilia shughuli za kilimo na ufugaji, anasema ni uamuzi wa busara aliofanya.

Mwalimu huyo hukuza kahawa, matunda aina mbalimbali, kuanzia ndizi, matundadamu (tamarillo), karakara, kati ya mengineyo.

Katika boma la Mwangangi lililoko eneo la Karatina, amewekeza katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na kuku.

Hata hivyo, kinachovutia mno katika mazingira yake ni ufugaji wa ndege wa umaridadi. Unapoingia kwa mwalimu huyo, mbali na sauti za kuku, kelele za ndege maridadi aina ya bantams, kanga na bata wa majini (mallards), zitakukaribisha au kukulaki.

Mwangangi aliingilia ufugaji wa ndege hao mwaka uliopita, 2019, uamuzi uliochangiwa na ziara katika boma la rafikiye eneo la Ruthagati, Nyeri. Ufugaji wa kuku, ana miaka kadhaa.

“Mazingira yake ni ya kuridhisha kutokana na ndege tofauti tofauti kama vile; njiwa, batamzinga, kanga, bata wa majini, bantams na bata wa nyumbani. Taswira iliyonikaribisha kwake ilichochea niige nyayo zake,” anaelezea mwalimu huyo mwenye ufasaha wa lugha ya Kiswahili.

Ndege aina ya bantams ndio walimsisimua zaidi kutokana na urembo wao. Isitoshe, Mwangangi anasema mradi wa ndege wa maridadi wa rafikiye huyo ni kitega uchumi.

“Kwa mfano, bei ya bantam mmoja haipungui Sh500, huku yai lake likiwa Sh100,” anadokeza.

Alianza kwa bantams tisa, na ingawa sita kati yao walifariki, anasema waliosalia wanaendelea kumtia tabasamu. “Nina mmoja, wa kike ambaye akianza kutaga mayai huendelea kwa muda wa miezi mitatu mfululizo,” anafichua.

Kwa sasa ana zaidi ya bantams kumi, na kulingana na mwalimu huyo oda ya mayai wa ndege hao ni tele, kiasi cha kulemewa kukithi kiu cha mahitaji ya wateja.

“Nikiweka chaki chini, nitakuwa na muda wa kutosha kupanua na kuimarisha mradi wangu wa ndege,” anasema, akifafanua kuwa wateja wa kuku ndio pia huagiza vifaranga wa ndege.

Kanga na bata wa majini, pia wanaendelea kumtia tabasamu mwalimu huyo, na anasema ni kwa muda tu vizimba vyake vijae ndege anaofuga. Fauka ya kuwa mfugaji chipukizi wa ndege, Mwangangi pia ameanza kufuga samaki, bidhaa ambayo bei yake inaendelea kupanda hasa kipindi hiki cha Covid-19.

Kimsingi, anasema anaendelea kujiandaa kustaafu, huku akiwa amesalia na mwaka mmoja pekee.

“Kwa walimu wenzangu ambao tutastaafu pamoja, ninawahimiza waanzishe miradi itakayowasaidia kujiendeleza kimaisha, mbali na pensheni tutakayopokea,” Mwangangi anashauri.

Uwekezaji katika sekta ya kilimo na ufugaji, nyumba au majengo ya kupangisha, uchukuzi, biashara, ni miongoni mwa miradi ambayo wengi huingilia ili kujipa pato la ziada.

“Ni muhimu kujipanga ukiwa katika ajira, weka akiba kidogokidogo kwenye vyama vya ushirika au akiba, ambayo pia unaweza kuitumia kupata mikopo kuwekeza katika miradi ya maendeleo,” anahimiza Jack Kamau, mtaalamu wa masuala fedha na kiuchumi.

Kulingana na Mwalimu Mwangangi, kilichomuwezesha kuafikia malengo yake, ni kujinyima mengi.

“Baada ya kukithi familia yangu riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi, mapato yanayosalia huyaelekeza katika miradi ya maendeleo ambayo pia hunisaidia kuweka akiba,” anafafanua, kwa tabasamu akidokeza kwamba amefanikiwa kusomesha wanawe hadi vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.