Bayern wapepeta Dortmund na kutua kwenye kilele cha jedwali la Bundesliga
Na MASHIRIKA
BAYERN Munich walirejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) baada ya kusajili ushindi wa 3-2 dhidi ya watani wao Borussia Dortmund mnamo Novemba 7, 2020, ugani Signal Iduna Park.
Kiungo na nahodha Marco Reus aliwaweka Dortmund uongozini kunako dakika ya 45 kabla ya beki David Alaba kusawazisha mambo sekunde chache baadaye.
Robert Lewandowski alishirikiana vilivyo na Lucas Hernandez na kufunga bao la pili la Bayern kabla ya sajili mpya Leroy Sane kufanya mambo kuwa 3-1 katika dakika ya 80.
Chipukizi Erling Haaland alimwacha hoi kipa Manuel Neuer mwishoni mwa kipindi cha pili na kufungia Dortmund goli la pili.
Lewandowski alidhania alikuwa amefungia Bayern goli la nne katika dakika za majeruhi baada ya mpira aliouelekeza langoni kumbabatiza chipukizi Jude Bellingham na kutikisa nyavu za wenyeji wao. Hata hivyo, goli hilo halikuhesabiwa na refa kwa madai kwamba fowadi huyo raia wa Poland alikuwa ameotea.
Hilo lilikuwa goli la pili la Lewandowski kukataliwa na refa baada ya kurejelea teknolojia ya video ya VAR kwa kuotea wakati wa gozi hilo.
Lewandowski kwa sasa amefunga mabao 13 kutokana na michuano minane iliyopita ligini dhidi ya Dortmund ambao ni waajiri wake wa zamani. Isitoshe, ndiye kwa sasa anayeshikilia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote katika soka ya Bundesliga.
Mbali na Lewandowski, sogora mwingine aliyeridhisha zaidi katika mechi hiyo ni fowadi chipukizi raia wa Ufaransa, Kingsley Coman aliyefungia Bayern bao la pekee na la ushindi dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu uliopita wa 2019-20.
Ushindi kwa Bayern ambao kwa sasa wameshinda mechi zao zote isipokuwa mbili za mwaka huu wa 2020, kwa sasa wamewaruka RB Leipzig na kutua kileleni mwa jedwali la Bundesliga kwa alama 18, tatu zaidi kuliko Dortmund wanaofunga orodha ya tatu-bora.
Hii ni mara ya kwanza tangu 2015-16 ambapo Bayern wameshinda mechi tano kati ya saba za ufunguzi kwenye kivumbi cha Bundesliga.