Habari

Tenda: Kampuni inayohusishwa na Joho yamulikwa

November 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

ALLAN OLINGO na DAVID MWERE

KAMATI ya Uchukuzi katika Bunge la Kitaifa inapanga kuchunguza kampuni inayohusishwa na familia ya Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, kwa madai ya kupokea kandarasi za Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) kwa njia za ufisadi.

Imedaiwa KPA imekuwa ikipendelea kampuni hiyo inapotoa zabuni za utoaji uhifadhi na usafirishaji wa mizigo bandarini.

Muungano wa Wafanyakazi wa Bandari (DWU) ndio ulikuwa umelalamika huku madai yakizuka kwamba kampuni hiyo ya Portside Freight Terminal Limited (PFTL) ilipewa zabuni ya kusimamia na kujenga kituo cha kisasa cha kupokea, kuhifadhi na kusafirisha shehena za nafaka.

Mbunge wa Pokot Kusini, Bw David Pkosing, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Uchukuzi katika Bunge la Kitaifa, Jumamosi alisema kamati yake inachunguza suala hilo na itamwita Katibu wa Wizara, Bw Solomon Kitungu kutoa ufafanuzi kuhusu madai hayo.

Pia usimamizi wa KPA, PFTL, na DWU utafika mbele ya kamati hiyo kutoa kauli zao kuhusu suala hilo tata ambalo limewakasirisha wafanyakazi wa bandari.

“Masuala ambayo yameibuliwa kwenye malalamishi yaliyowasilishwa bungeni na DWU ni mazito na yanafaa yashughulikiwe haraka. Kama kamati tunachunguza suala hili ili kuona iwapo PFTL inapendelewa na wizara jinsi inavyodaiwa,” akasema Bw Pkosing.

Mnamo Septemba 24, 2020, Karani wa Bunge la Kitaifa, Bw Michael Sialai alimwaandikia Bw Kitungu barua kuhusu masuala yaliyoibuliwa na wafanyakazi wa bandari japo kufikia jana, Bw Pkosing alisema hawakuwa wamepata jibu lolote kutoka kwa wizara.

“Haya ni masuala ambayo yanafaa kujibiwa haraka. Nashangaa kwa nini wizara inajikokota kuwasilisha majibu yao kwetu,” akaongeza Bw Pkosing.

Kaimu Mkurugenzi Msimamizi wa KPA, Bw Rashid Salim, kwenye ripoti yake iliyoonekana na Taifa Leo, alikiri kwamba walipata ombi kutoka kwa PFTL, kampuni hiyo ikitaka ipewe kibali cha kujenga kituo cha kisasa cha kupokea, kuhifadhi na kusafirisha shehena za nafaka.

“Walituma ombi la kupewa leseni ili wajenge kituo hicho kipya tena cha kisasa. Hata hivyo, madai kwamba walipendelewa hayana mashiko. Kandarasi iliyoafikiwa kati ya KPA NA PTFL ilifuata sheria zote za utoaji wa zabuni na ilinakiliwa kwenye nambari KPA/116/2005D,” akasema Bw Salim.

Kwenye ripoti yake kwa kamati hiyo, KPA ilisema PTFL ambayo zamani ilijulikana kama Hsye Investment Limited, ilipokezwa tenda hiyo kwa kuwa tangu mnamo 2015, imekuwa ikitumia kituo cha zamani kuhifadhi mizigo na kufuata utaratibu uliopo kwenye makubaliano ya kandarasi zao.

Katibu Mkuu wa DWU, Bw Simon Sang’ mnamo Septemba 7, 2020 aliandikia Bunge la Kitaifa akilalamikia oparesheni ya kimapendeleo ya kampuni ya PFTL bandarini kwa mkurugenzi wa KPA lakini hakuna hatua iliyochukuliwa hadi leo.

Masuala mengine yaliyoibuliwa na muungano huo wa wafanyakazi wa bandarini kando na KPA kudaiwa kupendelea PFTL, ni vifo vya wafanyakazi wawili na kujeruhiwa kwa wengine sita.