Michezo

Ronaldo afunga huku Juventus wakila sare na Lazio kwenye Serie A

November 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

FOWADI matata raia wa Ecuador, Felipe Caicedo alifunga bao katika dakika ya 95 na kusawazishia Lazio katika matokeo yaliyowanyima Juventus ushindi muhimu kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A) uwanjani Stadio Olimpico mnamo Novemba 8, 2020.

Caicedo alimwacha hoi kipa Wojciech Szczesny sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa. Bao hilo lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake ya Joaquin Correa.

Cristiano Ronaldo aliwaweka Juventus uongozini katika dakika ya 15 baada ya kukamilisha krosi ya Juan Cuadrado kwa ustadi mkubwa. Bao la Ronaldo lilikuwa lake la sita kutokana na mechi nne za Serie A.

Matokeo hayo dhidi ya Lazio yaliwasaza Juventus katika nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 13 sawa na Atalanta wanaofunga mduara wa nne-bora.

Kocha Andrea Pirlo na wanasoka wake wa Juventus watajilaumu wenyewe kwa utepetevu uliochangia sare hiyo dhidi ya Lazio ambao walicheza kwa tahadhari kubwa huku wakishindwa kabisa kumtatiza kipa Szczesny.

Lazio ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha Simone Inzaghi walipaa hadi nafasi ya tisa jedwalini kwa alama 11 sawa na Napoli na Hellas Verona.

Kabla ya kufunga bao, Ronaldo ambaye ni mchezaji wa zamani wa Manchester United na Real Madrid, alishuhudia makombora yake mawili langoni mwa Lazio yakigonga mhimili wa goli na jingine likipanguliwa na kipa Pepe Reina.

Nyota huyo aliondolewa uwanjani zikisalia dakika 15 kwa mechi kukamilika.