Makala

BURUDANI: Berin Bosibori Koroso, msanii wa nyimbo za Rhumba na Zouk

November 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

NI ndoto ya kila msanii kuona anaimarika katika sanaa yake na kutambulika kote duniani.

Berin Bosibori Koroso anahakikisha habaki nyuma ni miongoni mwa kina dada wanaopania kujizolea umaarufu si haba hapa nchini pia kimataifa akilenga kuibuka kati ya wanamuziki tajika. Anaamini anacho kipaji cha kutesa katika jukwaa la muziki na kufaulu kutuzwa miaka ijayo.

Katika mpango mzima anasema anatamani sana kuendeleza masuala ya muziki na kutinga upeo wa mwimbaji Susan Owiyo aliyejizolea umaarufu miaka iliyopita.

Dada huyu ni kati ya wanawake wachache hapa nchini wanaojivunia kughani nyimbo za burudani kwa mtindo wa Rhumba na Zouk.

”Natamani sana kuibuka kati ya wanamuziki bora nchini na kupata kazi za kutumbuiza katika majukwaa ya hadhi ya juu nchini pia katika mataifa ya kigeni,” alisema na kuongeza kuwa ingawa alianza utunzi wake miaka mitatu iliyopita ana imani tosha ipo siku kazi zake zitakumbalika katika tasnia ya muziki wa burudani.

Anasema alianza kujituma katika masuala ya muziki mwaka 2018 ingawa alitambua kipaji chake akiwa wa Shule ya Upili ya Kereri Girls.

Banana Love

Binti huyu anasema ametunga jumla ya fataki kumi lakini amefaulu kurekodi nyimbo nane za video. Nyimbo hizo zikiwa: ‘Smile’, ‘Wajua’ na ‘Banana Love’ ambazo zimerekodiwa Super Squad Production, ‘Baby Love’ (World Wave), ‘Obwanchani-Mapenzi’ (One Studio), kisha ‘Addictive’, ‘Need to pray’ na ‘Peke yako’ (zote Mastered Production).

Katika kile kinaodhihirishwa wazi kwamba msanii huyu ametunukiwa kipaji tosha katika muziki ndani ya miaka mitatu nyimbo zake mbili zimefaulu kupata mpenyo na kupepeushwa kupitia vituo tofauti vya runinga hapa nchini. Banana Love na Baby Love zimechezwa kupitia Citizen TV na K24 mtawalia.

Berin Bosibori Koroso; msanii wa nyimbo za Rhumba na Zouk. Picha/ John Kimwere

”Ingawa bado sijatambua wafuasi wangu wale wengi huwa wanaume ama wanawake sina budi kuwashukuru sana kwa kunipa sapoti,” akasema na kuongeza kuwa akiwa jukwaani mashabiki wake hupenda awaimbie kibao cha Banana Love.

Msanii huyu anasema hapa huvutiwa na wasanii wengi tu lakini anataja wawili kama Sanaipei Tande mtunzi wa ‘Kunitesa’ na ‘Najuta. Pia yupo Nyota Ndogo aliyetamba na kibao kama ‘Watu na Viatu’ pia ‘Subira.’

Kolabo

Kama ilivyo kawaida wa wanamuziki wengine dada huyu anasema angependa sana kufanya kolabo na msanii Ruby mtunzi wa kibao cha ‘Na Yule’ ambaye ni kati ya waimbaji ambao hufanya vizuri nchini Tanzania.

Chipukizi huyu anasema wasanii wengi hujikuta njia panda kwa vyombo vya habari nchini kutocheza nyimbo zao. Anashauri wenzie kutovunjika moyo mbali wazidi kukaza buti huku wakiamini siku moja milango itafunguka na kupata mwelekeo katika jukwaa la muziki wa burudani.