Mbinu bora za kukuza brokoli
NA PETER CHANGTOEK
BROKOLI (broccoli) ni mboga ya jamii ya kabeji, ambayo huchanua maua ambayo huliwa na binadamu. Hata hivyo, ni nadra sana kuwapata wakulimu wengi ambao huukuza mmea huo unaowewa kumfaidi mkulima. Sehemu za mmea huo ambazo huliwa na binadamu ni maua yake yenye rangi ya kijani kibichi pamoja na mashina.
Kwa mujibu wa Bi Carol Mutua, mhudumu katika idara ya mimea, mboga, maua na matunda na mchanga, katika Chuo cha Egerton, uzalishaji wa brokoli unaanza kushika kasi, kwa sababu ya uwezo wake wa kutibu.
“Pia kuna uhitaji unaoongezeka katika hoteli na supamaketi, na za kuuzwa nje ya nchi. Tatizo moja lililopo katika uzalishaji wa mmea huu ni kutohitajika kwa wingi na walaji kwa sababu wengi wao hawajui jinsi ya kupika,” asema Bi Carol.
Brokoli hukuzwa katika maeneo kadhaa nchini Kenya, kama vile; Kiambu, Nairobi, Laikipia, Murang’a, Makueni pamoja na sehemu kadhaa za Bonde la Ufa.
Mazingira ya ukuzaji
Kwa mujibu wa Bi Carol, halijoto (temperature) yafaa iwe chini kwa ukuaji na ubora unaohitajika na brokoli. “Joto jingi linaweza kuzuia kuundwa kwa ‘vichwa’. Kuwepo kwa baridi ya nyuzijoto iliyo chini ya 10 baada ya kupandwa, husababisha maua kutokea kabla ya wakati unaofaa, na hivyo kusababisha kuundwa kwa vichwa vidogo,” aongeza mtaalamu huyo.
Nyuzijoto mwafaka ni kati ya 13.9 na 20, na zaidi ya 20, ubora wa brokoli hudorora. Bi Carol anatahadharisha kuwa halijoto ikipita nyuzijoto 25, huenda vichwa visiundwe kabisa kwa mmea huo.
Mchanga ulio na uwezo wa kuyahifadhi maji ni mwafaka kwa ukuzaji wa brokoli. Aidha, brokoli huhitaji mchanga wenye kiwango cha tindikali na alkali cha 5.5-6.5 (pH). Mmea huo unayahitaji maji ya kutosha kwa ajili ya ukuaji bora. Hivyo basi, endapo mvua ya kutosha haipo, ni jambo aula kuwapo kwa maji ya kutumiwa kunyunyizia kwa mimea hiyo.
“Brokoli huhitaji elementi ijulikanayo kama Molybdenum kwa wingi. Molybdenum hukosekana kwa mchanga wenye tindikali iliyo chini ya 5.5,” asema, akiongeza kwamba ukosefu huo wa elementi hiyo unaweza kukabiliwa kwa kutia mbegu katika dawa zifaazo.
Mimea hiyo inaweza kupandwa moja kwa moja kwa shamba lililotayarishwa, na pia mbegu za mmea huo zinaweza kuoteshwa kwanza katika kitalu, kabla ya kuhawilishwa. Miche ya brokoli huhawilishwa kutoka kwa kitalu baada ya kuchukua muda wa wiki nne hadi sita. Pia, inaweza kuhawilishwa ikiwa imetimiza kimo cha sentimita 8 hadi 10, au ikiwa na majani matatu au manne yaliyokua kwa ukamilifu.
Wakati wa kupanda, nafasi ya sentimita 45 hadi 90 huachwa kutoka kwa mmea mmoja hadi mwingine baina ya laini, na sentimita 30 hadi 60 kutoka kwa mmea mmoja hadi mwingine katika laini.
Brokoli huhitaji madini ya nitrojeni na ‘potassium’ kwa wingi. Mbolea zenye madini ya fosiforasi (phosphorous) na ‘potassium’ zafaa kumwagiwa shambani kabla ya kuhawilishwa kwa miche. Baada ya kuihawilisha miche hiyo, mbolea zenye nitrojeni hutumiwa, baada ya muda wa wiki nne. Hali kadhalika, baada ya wiki nyingine tatu, mbolea hiyo hiyo, yenye nitrojeni, hutumiwa kwa mimea hiyo.
Kiwango cha mbolea aina ya CAN kinachotumika ni gramu 5-10 kwa mmea mmoja, au kilo 185-370 kwa hekta na kilo 200 za DSP kwa hekta.
Brokoli zina mizizi isiyoingia ndani ya mchanga kwa kina kirefu sana. Hivyo basi, zinapoendelea kukua, zahitaji unyevuunyevu. Mimea hiyo inapoendelea kukua shambani, ni jambo aula kuhakikisha kuwa magugu yanaangamizwa ile yasije yakayafyonza maji ambayo yanafaa kutumiwa na mimea.
Mkulima anaweza kutumia viuagugu (herbicides) kuyaangamiza magugu. Aidha, aweza kuugubika mchanga katika mahali ambapo brokoli zinamea, kwa kutumia nyasi pamoja na majani yaliyokauka, kusudi kusaidia kuzuia kuota kwa maotea na kuyahifadhi maji mchangani pia.
Katika ukulima huo wa brokoli, wadudu waharibifu huenda wakaivamia mimea hiyo. Mkulima hana budi basi, kutumia viuadudu (pesticides) kuwakabili wadudu hao.
Pia, mkuzaji anaweza kuipanda mimea fulani ambayo huwafukuza baadhi ya wadudu waharibifu. Wadudu kama vile bungo (beetle), husaidia kuwaangamiza baadhi ya wadudu waharibifu shambani.
Mbali na changamoto ya mimea kuviziwa na wadudu, mkulima pia atahadhari dhidi ya magonjwa mbalimbali, ambayo huathiri mimea aina ya brokoli. Anafaa kujua aina mbalimbali za magonjwa na jinsi ya kuzuia au kuyakabili.
Endapo ni maradhi yanayosababishwa na kuvu, basi atumia viuakuvu (fungicides), n.k. Baada ya kuhawilishwa kutoka kwa kitalu hadi shambani zinakopandiwa, brokoli huchukua siku 45 hadi 60 ili zikomae na kuwa tayari kuchumwa.
Ushauri
BROKOLI ni mboga ya jamii ya Brassica Oleracea, kundi linalojumuisha mboga kama vile kabeji, sukumawiki, koliflawa (cauliflower) n.k. Huweza kukuzwa katika maeneo tofauti tofauti ya taifa la Kenya, mathalani; Kiambu, Nairobi, Laikipia, Murang’a, Makueni, miongoni mwa mengine.
Katika maeneo yasiyopokea mvua ya kutosha, brokoli hunyunyiziwa maji ili kuboresha mazao.
Mkulima aweza kupanda mimea takribani 15,000 kwa shamba ekari moja na tani 12 hadi 17 zaweza kuchumwa kwa ekari moja. Brokoli huwa na uzani wa gramu 350-400. Mbegu aina tofauti za mmea huo zapatikana katika maduka mengi ya kuuza mbegu. Mimea hiyo huchukua siku 45-60 baada ya kuhamishwa kutoka kwa kitalu, ili ikomae.
Manufaa
Zina nyuzi zinazosaidia kumeng’enywa kwa chakula tumboni. Aidha hupunguza kolestero (cholesterol) mwilini. Isitoshe, huimarisha ngozi. Aidha, zina madini ya kalisiamu (calcium), ‘potassium’, Vitamini C, n.k. Hali kadhalika, mboga hizo zina chembechembe ambazo husaidia kupunguza uwezekano wa kukabiliwa na maradhi ya saratani.
Vilevile, wataalamu wanadokeza kwamba brokoli husaidia kuyapa macho kinga dhidi ya maradhi fulani.