Nahodha wa Starlets apata hifadhi Thika Queens
Na CHRIS ADUNGO
BAADA ya uhamisho hadi Yanga Princess ya Tanzania kugonga ukuta, nahodha wa Harambee Starlets Dorcas Shikobe amepata hifadhi mpya kambini mwa Thika Queens wanaoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake nchini Kenya (KWPL).
Amerasimisha uhamisho wake hadi kambini mwa kikosi hicho kwa kutia saini mkataba wa miaka mitatu.
Shikobe alichezea Oserian Ladies katika Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) mnamo 2019 kabla ya kuagana na kikosi hicho kilicho na makao makuu mjini Naivsha.
Meneja wa timu ya Thika Queens, Fredrick Chege amefichua kwamba Yanga walishindwa kuheshimu maagano yao ya awali nao ndiposa uhamisho wa Shikobe utatibuka katika dakika za mwisho mnamo Oktoba.
“Yanga walitarajiwa kumpokeza Shikobe kima cha Sh100,000 za kutia saini mkataba. Walitazamiwa pia kulipa ada ya Sh200,000 za uhamisho. Lakini badala yake, walisema wangempa mwanasoka huyo Sh50,000 pekee kisha kukamilisha salio baadaye. Tulionelea kwamba hawakuwa na haja sana huduma za Shikobe,” akasema Chege.
Chege alisema hali sawa na hiyo ilishuhudiwa wakati wa kusajiliwa kwa beki Wincate Kaari aliyetua kambini mwa Yanga Princess kabla ya matumaini yake ya kuchezea kikosi hicho kuvunjika ghafla na akalazimika kupiga abautani alipotambua kwamba hakuwa amewekewa fedha za kutia saini mkataba mpya kwenye akaunti yake ya benki.
“Kaari yuko nasi kwa sasa na anashiriki mazoezi na wanasoka wenzake. Kwa upande wake, Shikobe anarejea katika kikosi alichoagana nacho kabla ya kuingia Oserian mnamo 2015. Tunajivunia sana huduma zao na tunatarajia makuu kutoka kwao baada ya kampeni za msimu huu kufunguliwa rasmi mnamo Novemba 28,” akasema Chege kwa kusisitiza kwamba Thika Queens wana kiu ya kurejesha ubingwa wa KWPL walioutwaa mara ya mwisho mnamo 2017.
“Hatujaagana na mchezaji wetu yeyote muhula huu. Safu yetu ya ulinzi iliyumba sana msimu jana. Lakini kuwepo kwa Shikobe na Kaari sasa kutaimarisha mambo hasa ikizingatiwa kwamba watashirikiana vilivyo na Nelly Sawe na Lydia Akoth,” akaeleza Chege.
“Tumechoka kumaliza kampeni za ligi kuu nyuma ya Vihiga Queens kwa muda mrefu. Huu ndio msimu ambao tumepania kurejea kileleni mwa jedwali la KWPL,” akaongeza.
Thika Queens wameratibiwa kufungua kampeni zao za KWPL msimu ujao dhidi ya limbukeni wa ligi hiyo, Ulinzi Starlets.